Home BIASHARA NMB, DART wapanda miti 1,000 Barabara ya Mwendokasi

NMB, DART wapanda miti 1,000 Barabara ya Mwendokasi

Google search engine

NA MWANDISHI WETU

KAMPENI ya Upandaji Miti Milioni 1 kwa mwaka 2023 iliyozinduliwa Jijini Dodoma na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ikiendeshwa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), imezidi kushika kasi baada ya miti 1,000 kupandwa jana pembezoni mwa Barabara ya Mabasi ya Mwendokasi jijini Dar es Salaam (DART). 

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashimu Komba, alizindua awamu ya kwanza ya upandaji miti kwenye ushoroba wa DART, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, CPA Amos Makalla, ambaye aliwaagiza Watendaji wa Serikali za Mitaa, Kata na Madiwani kushiriki utunzaji wa miti hiyo katika maeneo yao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, DC Komba alisema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inawapongeza NMB kwa kuishirikisha DART katika upandaji miti huo, unaolenga kustawisha Jiji la Dar es Salaam, ambalo linaendesha Kampeni ya Usafi wa Mazingira iitwayo; ‘Safisha, Pendezesha Dar’ inayofanywa na RC Makalla.

“Mheshimiwa Makalla amenituma kufikisha salamu za pongezi kwenu DART na NMB kwa kampeni hii ya kutunza mazingira kwa ustawi wa Viumbe Hai wakiwemo binadamu. Jijini Dar es Salaam, mlianzia Kigamboni, mkaja Bunju na leo mko Ubungo kwa lengo la kupanda miti 1,000 katika ushoroba wa DART.

“Yeye binafsi amekuwa na kampeni ya ‘Safisha, Pendezesha Dar,’ ambayo imemsukuma kusafirisha viongozi mbalimbali kwenda Kigali nchini Rwanda kujifunza masuala yanayohusiana na usafi wa mazingira, ndio maana anawapongeza kwa kumuunga mkono yeye na Makamu wa Rais, Dk. Mpango,” alisema DC Komba.

Aliongeza kwa kuitaka DART ambao ndio wenyeji wa hafla hiyo. kuzishirikisha Ofisi za Watendaji wa Mitaa, Kata na Madiwani wa maeneo yote yanayopitiwa na mradi wa DART, kuhakikisha wanashiriki mchakato wa kuitunza miti na kuilinda kutokana na watumiaji wengine wa barabara hizo.

“Viongozi wa kada zote hizo na wafanyakazi Serikalini wanapaswa kuhakikisha kunakuwepo na matumizi sahihi ya kila eneo, wafanyabiashara wajue mipaka yao, waenda kwa miguu halikadhalika, ili kuifanya miti hiti hii kutofikiwa na shughuli za kibinadamu na kuathiri ukuaji wake,” alisisitiza Komba.

Awali, Afisa Mkuu wa Biashara na Wateja Binafsi wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki yake inatambua na kuthamini mazingira na ndio maana wakatenga kiasi cha Shilingi Bilioni 2 kutokana katika faida yao ya Sh. Bilioni 429 waliyopata mwaka jana, ili kufanikisha kampeni hiyo muhimu.

“NMB tumekuwa na utamaduni wa kutumia asilimia moja ya faida yetu kwa mwaka kusaidia Sekta za Elimu, Afya na Majanga, lakini mwaka huu ambao tulipaswa kutumia Shilingi Bilioni 4.2, Bodi ya Wakurugenzi ikaidhinisha Sh. Bil. 2 za ziada zielekezwe katika mazingira, hivyo tutatumia Sh. Bil. 6.2.

“Tunaamini katika ahadi ya Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Edwin Mhede kuwa miti 1,000 inayopandwa katika ushoroba wa DART itatunzwa kwa asilimia 100. Nasi kwa kutambua umuhimu wa elimu ya mazingira, tukatenga Sh. Milioni 472 kama zawadi kwa shule 189 zinazoshiriki Shindano la ‘Kuza Mti Tukutuze.’ 

Alifafanua kuwa, shule bora katika upandaji wa miti 2,000 na ikaitunza kwa asilimia 80, itazawadiwa Sh. Mil. 50, huku shule ya pili miongoni mwa zitakazopanda miti 1,500 na kuitunza kwa asilimia 80, italamba Sh. Mil. 30, huku shule ya tatu kati ya zitakazopanda miti 1,000 na kustawisha asilimia 70, itabeba Sh. Mil. 20.

Kwa upande wake, Dk. Mhede aliishukuru NMB kwa kuishirikisha DART katika kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais Dk. Mpango ya kutaka mamlaka zote za Serikali, taasisi na mashirika ya umma kujikita katika kampeni hiyo inayolenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Shukrani NMB kwa wazo bunifu la kuja na kampeni hii, ambayo kwetu sisi DART ni fursa ya kutuwezesha kurejesha uoto wa asili katika ushoroba wa barabara zetu, ambao unaondolewa na ujenzi wake. Kampeni hii itatusaidia kurejesha uhalisia wa maeneo yetu. 

“Tumejipanga kuitunza miti hii, jukumu ambalo nalikabidhi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ulinzi wa Miundombinu ya DART (China-Tanzania Security), El-Malick Aboud, ambaye atashirikiana na watendaji wa mitaa, kata zinakopitiwa na mradi wa mwendokasi kote Dar es Salaam.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Washauri ya DART, Florance Turuka, aliishukuru NMB kwa kuwapa fursa ya kushirikiana nao katika upandaji miti kwenye ushoroba wa kilomita 20.6 wa barabara za mwendokasi, mradi ambao utajumuisha kilomita 154.4 pindi zitakapokamilika awamu mbili za barabara za Mbagala na Gongolamboto.

“Tunapokea kutoka NMB na TFS miche 1,000 ya miti, tunaipanda leo kuanzia Ubungo kuelekea Kata za Manzese na Magomeni, huku tukiahidi kuitunza ipasavyo kama alivyosema Dk. Mhede, kwani lengo letu sisi DART – ambao tunasafirisha abiria kupitia kaulimbiu ya ‘Usafiri wa Umma Nadhifu,’ kuitunza kwa asilimia 100,” aslisitiza.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here