Home BIASHARA AFCFTA KUONGEZA MAUZO YA NJE NA KUBORESHA UWIANO WA BIASHARA

AFCFTA KUONGEZA MAUZO YA NJE NA KUBORESHA UWIANO WA BIASHARA

Google search engine

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil Abdallah amesema utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) katika kuondoa vikwazo visivyokuwa vya kiushuru na kufungamanisha Sera za Biashara kutachangia kuongeza mauzo ya nje, kuboresha uwiano wa biashara, kupatikana kwa soko la bidhaa za Tanzania nje ya Nchi na kukuza biashara na uchumi kwa ujumla

Dkt. Abdallah ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 17 Makatibu Wakuu wa AfCFTA unaofanyika kuanzia Juni 18 – 22, 2024 ukifuatiwa na Mkutano ngazi ya Mawaziri utakaofanyika Juni 24 – 25, 2024, Zanzibar, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Mikutano ya ngazi zote kwa mwaka 2024.

Aidha, Dkt. Abdallah amebainisha kuwa utekelezaji wa AfCFTA nchini kutachangia kuhamasisha ukuaji wa Viwanda na kuboresha mazingira ya biashara ambako kutatoa matokeo chanya kwa kuongeza ajira, kuongeza Pato la Taifa na kutoa huduma bora za kijamii kwa Watanzania na hatimaye kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2025 na Agenda 2063 ya Afrika tunayoitaka.

Vile vile, ametoa wito kwa Jumuiya za Wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za soko la AfCFTA lenye watu zaidi ya billioni 1.3 kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vinavyotakiwa zinazoweza kushindana katika soko hilo ili kutekeleza kwa vitendo Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufungua nchi kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji.
`
Wenzetu wanakimbia, sisi tunatakiwa kukimbia zaidi, ni jukumu letu sasa kama Watanzania kuchangakia fursa zilizopo katika Mkataba wa AfCFTA na hapo ndipo tutakuwa tunatekeleza kwa vitendo ile Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake katika kufungua nchi kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji”. Amesema Dkt Abdallah.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Bi Fatma Mabrouk Khamis amewashauri Makatibu Wakuu hao wa Biashara kuhakikisha wanatimiza malengo ya AfCFTA katika kuunda Afrika yenye ustawi na jumuishi ili kuhakikisha wananchi wa kila Nchi wananufaika na Manufaa ya AfCFTA yanagawanywa kwa usawa bila kuacha Nchi Mwananchama yoyote nyuma.

Aidha, ametoa wito kwa Wananchi wote hususani Wananwake na Vijana wa Tanzania Bara na Visiwani kuchangamkia fursa hizo kwa kuuza bidhaa zenye ubora na uasili wa Tanzania kulingana na mahitaji ya soko hilo linalojumisha Nchi 54 za Afrika ili kuongeza ajira, kwa kuwa AfCFTA inatoa fursa ya kuuza bidhaa au huduma ndani ya Bara la Afrika bila vikwazo vyovyote vya kiushuru kwa Nchi yoyote Afrika ambayo ni Mwanachama.

Akitoa mfano wa bidhaa za mwani zinazotengenezwa kwa Wingi Zanzibar, Bi Khamis amesema kutokana na fursa za AfCFTA, bidhaa hizo zinauzwa Uganda, Congo na Nchi nyingine za Afrika na kuwa Kampuni zinazosafirisha bidhaa hizo zimepatiwa mafunzo ya kuelewa mahitaji ya soko na kuhakikisha bidhaa zao zinafikia viwango vinavyohitajika.

Mkataba huu wa AfCFTA unatulazimisha Nchi za Afrika kuboresha mazingira ya biashara, kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru, kujenga miundombinu na kuboresha sheria zetu ili kupanua wigo wa soko, kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta mbalimbali kama vile viwanda, kilimo, mifugo na ufugaji, hali ambayo inaongeza ajira, Pato la Taifa na kukuza uchumi wa wananchi wetu na wa Taifa kwa ujumla” Amesema Bi Khamis.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Biashara,Uwekezaji, Haki miliki Bunifu na Biashara Mtandao wa AfCFTA Bi Emily Mburu Ndoria amesema AfCFTA imetengeneza Itifaki ya Biashara ya Bidhaa, Biashara ya Huduma, Uwekezaji, Haki Miliki Bunifu, Biashara Mtandao, Biashara ya Vijana na wanawake zinazolenga kurahisisha utekelezaji wa AfCFTA kwa ujumla kwa kuiwezesha Afrika kufanya biashara baina ya Nchi na Nchi na kukuza uchumi wake.

Aidha, amezishauri Nchi wananchama kuhamasisha wananchi wao hususani Wananwake na vijana kutumia fursa zinazopatikana katika Mkataba wa AfCFTA kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa ili ziweze kukidhi mahitaji na kushindana katika soko hilo muhimu la Afika.

Mkutano huo umejumuisha Maafisa Biashara Waandamizi (STOs) kutoka nchi wanachama wa AfCFTA na Jumuiya za Kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Kati (ECCAS), Shirika la Kikanda la Maendeleo kati ya Serikali (IGAD), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), Jumuiya ya Nchi za Sahel-Sahara (CEN-SAD,) Tume ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA), Umoja wa nchi za Kiarabu wa Maghreb (UMA) na Benki ya Uagizaji na Usafirishaji nje Bidhaa za Afrika (AFREXIMBANK)

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here