Home MICHEZO BENKI YA NMB YAZIPA VIFAA VYA MILIONI 13/- TIMU JWTZ ZINAZOSHIRIKI BAMATA...

BENKI YA NMB YAZIPA VIFAA VYA MILIONI 13/- TIMU JWTZ ZINAZOSHIRIKI BAMATA 2023

Google search engine

NA MWANDISHI WETU

KATIKA mashindano ya Baraza la Majeshi la Tanzania (BAMATA) yalioanza kutimua vumbi Alhamisi Februari 9 mjini Mtwara, Benki ya NMB imekabidhi msaada wa jezi  za michezo mitano kwa timu za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Bara na Zanzibar, zenye thamani ya Sh Miloni13.

Makabidhiano hayo yamefanyika Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, ambako Mwakilishi wa Kurugenzi ya Michezo JWTZ Bara, Kanali John Thomas Nyanchoha na Luteni Kamanda Ali Mgeni Amour wa JWTZ Zanzibar, walipokea vifaa kutoka kwa Meneja Mwandamizi wa benki hiyo, Queen Kinyamagoha.

BAMATA 2023 yanatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mjini Mtwara, na yatahitimishwa Februari 22 mwaka huu, ambako Majeshi ya Ulinzi, Usalama, Magereza na Polisi, watachuana vikali katika michezo ya mpira wa miguu, mikono, wavu, netiboli, kikapu, riadha na mingineyo.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa wawakilishi hao wa JWTZ – Bara na Zanzibar, Kinyamagoha alisema NMB inajivunia ushirikiano wake na Majeshi mbalimbali nchini na kwamba wanaamini msaada wao mwaka huu utakuwa na tija kwa timu hizo kufanya vizuri na kutwaa makombe.

“NMB ni wadau wakubwa wa JWTZ, ambako tumekuwa tukitoa vifaa mbalimbali wanaposhiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa, huku pia tukidhamini shindano la gofu la Mkuu wa Majeshi (CDF Trophy). Tunawatakia ushiriki mwema na wenye mafanikio, huku tukiahidi kudumisha ushirikiano baina yetu,” amesema Kinyamagoha.

Meneja huyo alisema siri ya benki yake kusapoti JWTZ ni kutokana na kutambua thamani ya jeshi hilo kwa taasisi yake, ikiwa ni pamoja dhamira ya kuchangia uimarishaji wa afya na kuhamasisha mafanikio kwa wanamichezo kutoka jeshi hilo.

Kwa upande wake, Luteni Kamanda Nyanchoha, kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, aliishukuru NMB kwa namna inavyojitoa kusapoti timu za JWTZ, huku akifafanua kuwa msaada wao huo umeipunguzia mzigo taasisi hiyo na kuahidi kuutumia vema kama chachu ya ushindi katika BAMATA 2023.

Naye SSP Mariam Simon, mbele ya Luteni Kamanda Ali Mgeni Amour wa JWTZ Zanzibar, alisema wamejipanga vya kutosha kutwaa makombe mbalimbali kwenye BAMATA 2023 na kwamba watapokuwa wanatoka mashindanoni Mtwara, watapitia NMB Makao Makuu, Dar es Salaam kuyaonesha kwa Menejimenti na Wafanyakazi wa NMB.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here