Home BIASHARA Benki ya NMB yanyakua tuzo 3 katika Annual Tanzania Service Excellence Awards...

Benki ya NMB yanyakua tuzo 3 katika Annual Tanzania Service Excellence Awards 2024

Google search engine

Na Mwandishi Wetu

Benki ya NMB imeshinda tuzo tatu katika tuzo za Annual Tanzania Service Excellence Awards 2024 zilizofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki  huku benki hiyo kutangazwa mshindi wa jumla wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika kampuni zinazofanya kazi nchini.

Benki hiyo pia ilijishindia tuzo baada ya kuibuka mshindi wa pili katika Sekta ya kibenki na mshindi wa pili katika kipengele cha mpango maalum na jumuishi wa huduma kwa wateja.

Tuzo hizo zilizoandaliwa na Taasisi ya Chartered Institute of Customer Management zilitambua dhamira ya Benki ya NMB katika utoaji huduma bora na kubadilisha maisha ya watu kwa kutoa huduma wezeshi kijamii na kiuchumi.

Tuzo za Service Excellence Awards zilianzishwa mnamo mwaka 2010 na zimekuwa zikifanyika katika nchi mbalimbali Barani Afrika lakini zimefanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Abella Tarimo alisema tuzo hizo ni uthibitisho wa utekelezaji mzuri wa mkakati wa benki hiyo.

“Katika Benki ya NMB, kuridhika kwa mteja ndio msingi wa shughuli zetu ndiyo maana huwa tunamtanguliza mteja wetu. Tuliboresha mifumo yetu mwaka jana ili kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bila changamoto. Kituo chetu cha huduma kwa wateja sasa kinafanya kazi saa 24 tangu Januari mwaka huu na yote haya yanaonyesha jinsi gani tumejizatiti katika kuendelea kumhudumia mteja wetu”.

Aliongeza, “Kupitia ubunifu wetu wa masuluhisho ya kidijitali, mtandao mpana wa matawi, na wafanyakazi wanaojitolea, tutaendelea kuchangia katika ukuaji wa sekta ya kifedha nchini na kutoa huduma za kipekee kwa wateja wetu pamoja na kuendeleza  utekelezaji wa mkakati wa benki wa Uwajibikaji Kwa Jamii (CSI). “

Balozi John Ulanga, Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Kushoto) akikabidhi cheti Mkuu wa idara ya  Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB, Abella Tarimo (wapili kushoto) wakati wa hafla ya utoaji tuzo za Annual Tanzania Service Excellence Awards 2024 zilizofanyika jijini Dar es Salaam ambapo benki hiyo ilinyakua jumla ya tuzo tatu. Katikati ni Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam Dismas Prosper. 

Balozi John Ulanga, Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema muundo wa uchumi wa Tanzania umebadilika kwa kiasi kubwa miaka 30 iliyopita.

“Miaka 30 iliyopita, asilimia 48 hadi 50 ya Pato la Taifa (GDP) ilichangiwa na kilimo na sekta ya huduma ilichangia karibu asiliia 25 tu. Leo, karibu asilimia 50 ya Pato la Taifa linachangiwa na sekta ya huduma,” alisema.

Aliongeza, “Katika muundo sahihi wa nchi ya kipato cha kati, asilimia 50 ya Pato la Taifa kuchangiwa na sekta ya huduma, asilimia 20 au chini ya kuchangiwa na kilimo na asilimia 30 iliyobaki inachangiwa na sekta ya uzalishaji na nyinginezo”.

Ulanga wakati wa hafla hiyo alizitaka kampuni kuwekeza katika tekinolojia ili kuboresha huduma kwa wateja huku akisisitiza kuwa uwekezaji katika tekinolojia unarahisisha utendaji kazi.

“Huduma bora inatofautisha kampuni moja na nyingine. Wakati ni sasa kwa kampuni kuangazia jinsi zinavyoweza kuongeza utoaji wa huduma bora kwa wateja,” aliongeza.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here