Home KITAIFA WAJASIRIAMALI WAHIMIZWA KURASIMISHA BIASHARA BRELA

WAJASIRIAMALI WAHIMIZWA KURASIMISHA BIASHARA BRELA

Google search engine
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, akisalimia na viongozi wa BRELA mara baada ya kuwasili katika eneo la Mlimani City kwa ajili ya kufungua mkutano wa wajasiriamali
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba, akizungumza katika mkutano huo

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Hashim Komba amewataka wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, (BRELA) na wadau wake kutumia fursa hiyo kurasimisha biashara zao ili biashara zao ziweze kukua.

Komba ametoa rai hiyo  Oktoba 24, 2023 wakati akifungua Maonesho ya kwanza ya BRELA na wadau wake, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Wito wangu kwenu BRELA na wadau wengine wa maonesho haya ni kwamba tuhakikishe hawa wajasiriamali mbalimbali wanakua, hivyo wasaidiwe kwa kupatiwa elimu ili waweze kurasimisha biashara zao,” amesema Komba.

Amesema ili kuboresha zaidi maonesho haya BRELA iendelee kuandaa maonesho kama haya katika maeneo mengine yatakayowezesha wadau wengi zaidi kufikiwa.

Ameyataja maeneo ambayo yana idadi kubwa ya wajasiriamali katika Wilaya ya Ubungo kuwa ni Mbezi na Manzese, hivyo BRELA itoe kipaumbele kwa kuwapatia elimu kupitia maonesho kama haya.

Pia ameitaka BRELA kuimarisha mahusiano na mazuri na taasisi zingine za Serikali hususan Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Serikali za Mitaa ambazo ndizo zinazowakutanisha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

Mhe. Komba amesema Maonesho haya pia yatumike kufanya tathmini ya huduma zinazotolewa sambamba na kuwa na madawati yanayowakutanisha wadau ili kupunguza watu wa kati (Vishoka) ambao wamekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara.

“BRELA, Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango Tanzania(TBS) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) shirikianeni katika utoaji wa elimu ili kudhibiti na kupambana na Bidhaa bandia, kuthibitisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali na kuhakikisha wanafanya sajili mbalimbali na kupata leseni,” amesema Mhe. Komba.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA itaendelea kuwahamasisha wadau wake kurasimisha biashara zao kupitia majukwaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki katika maonesho.
Maonesho ya BRELA na wadau wake ambayo yatahitimishwa na mkutano wa Wadau tarehe 27 Oktoba, 2023 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Da es Salaam, kauli mbiu yake ni “Urasimishaji Bashara katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.”

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here