Home KITAIFA NMB yawezesha wakulima Tabora kulipwa fidia kwa wakati

NMB yawezesha wakulima Tabora kulipwa fidia kwa wakati

Google search engine
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Burhan (wa tatu kushoto) akipokea mfano wa hundi ya zaidi ya Shilingi milioni 374 , kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Nsolo Mlozi (watatu kulia) kwa ajili ya fidia ya wakulima wa tumbaku walioharibiwa mazao yao na mvua kwa msimu wa 2022/2023 kwenye hafla iliyofanyika mkoani Tabora. Wanaoshuhudia ni Meneja wa Mamlaka ya Bima kanda ya Magharibi, Dk. Lupilya Emmanuel (wa pili kushoto), Afisa Mkuu wa Fedha wa kampuni ya Bima ya UAP, Nelson Rwihula(kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Tumbaku Mtapenda, Deogratius Richard(kushoto).
 

Na MWANDISHI WETU

-TABORA

Benki ya NMB imesaidia wakulima wa tumbaku zaidi ya 400 mkoani Tabora kulipwa kwa wakati fidia ya hasara waliyopata baada ya mashamba yao kuharibiwa na mvua kubwa za mawe mwezi Januari na Mei mwaka huu.

 Hundi ya malipo ya madai hayo ya kiasi cha Shilingi milioni 374 kutoka kampuni ya bima ya UAP Insurance imekabidhiwa jana kwa Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dk. Batilda Salha Burhani aliyesema kuwa fidia hizo ni kubwa kuwahi kulipwa wakulima wengi nchini kwa wakati mmoja.

 “Ushiriki wa NMB katika kulikamilisha hili kwa haraka kunaifanya kuwa zaidi ya benki katika kulihudumia taifa,” Dkt Burhani alibainisha na kusema kuwa hilo linaendana na azma ya serikali kuhakikisha wakulima wote nchini wana bima.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa wakulima waliokatia mashamba yao bima dhidi ya majanga walifanya maamuzi sahihi kwani bima hizo zimekuwa mkombozi wao na sasa wataweza kuendelea na shughuli zao wakiwa na uhakika wa maisha.

 Dk. Batilda alizishukuru Benki ya NMB na UAP kwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wakulima hao wanalipwa madai yao kwa wakati huku akisema hilo linaendana na azma ya Serikali kuwaunga mkono wakulima na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

 “Juhudi za kuhakikisha fidia hii inalipwa kwa haraka si tu zinafanya waathirika kuendelea na kilimo chao lakini pia zinawapa imani na bima na kuwaonyesha umuhimu wa kuwa na kinga dhidi ya majanga hasa kupitia kubima na NMB,” alisema huku akisisitiza umuhimu wa zao la tumbaku katika maendeleo ya wakulima binafsi na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa Benki ya NMB, Nsolo Mlozi, amesema Benki ya NMB inaunga mkono juhudi za Serilaki kuhakikisha kilimo nchini kinakuwa na tija na kuwanufaisha wakulima.

 Amesema benki yao na Serikali ni wadau wakubwa wa maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na wananchi wote kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mlozi, NMB inathamini umuhimu wa kilimo cha kisasa na mchango wa zao la tumbaku katika ujenzi wa taifa ndiyo maana ina ushirika na wadau mbalimbali ili kuwasaidia wakulima na sekta ya kilimo.

 “Ni kwa msingi huo ndio maana tumeishughulikia changamoto ya malipo ya wakulima wa tumbaku wa Tabora iliyotokana na uhaba wa hivi karibuni wa dola katika uchumi wetu,” mtaalamu huyo wa kilimo biashara alibainisha.

Aidha, alisema mara tu baada ya wakulima hao kufikwa na madhira hayo, Benki ya NMB na Kampuni ya UAP walifanya upembuzi stahiki na tathmini ya kina kuona ni fidia kiasi gani inastahili kwa uharibifu wa mashamba husika.

 Mwakilishi wa UAP, Mariam Hussein, aliwaambia walioshiriki katika makabidhiano hayo kuwa lengo la kushirikiana na NMB ni kuhakikisha kuwa huduma za bima zinachangia kikamilifu kuendeleza kilimo na kuleta maendeleo ya uchumi nchini.

Google search engine
Previous articleRAIS SAMIA ATUA JIJINI LUSAKA, ZAMBIA KWA ZIARA YA KITAIFA
Next articleWAJASIRIAMALI WAHIMIZWA KURASIMISHA BIASHARA BRELA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here