Home KITAIFA SERIKALI KUKAMILISHA UJENZI WA NYUMBA 5,000 MSOMERA NDANI YA MIEZI SITA

SERIKALI KUKAMILISHA UJENZI WA NYUMBA 5,000 MSOMERA NDANI YA MIEZI SITA

Google search engine
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax akiongea na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Geophrey Pinda wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba 5,000 za wakazi wa Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga.
Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakiendelea na ujenzi wa nyumba za wakazi wa Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga waliohama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Arusha.
Muonekano wa eneo la kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga walipo hamishiwa kwa hiari wakazi wa jamii ya kifugaji kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Arusha.

Na HASSAN MABUYE

-HANDENI TANGA

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax amesema Serikali inataraji kukamilisha ujenzi wa nyumba 5,000 ambazo zimeanza kujengwa za Wakazi wa Msomera Wilayani Handeni mkoa wa Tanga waliohama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Dk. Tax ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa katika kijiji cha Msomera mkoani Tanga akiongozana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Geophrey Pinda.

“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba nyumba 1,000 zinakamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2023 na tutaendelea kuzikabidhi nyumba kadri zinavyokwisha, lakini nyumba 5,000 zinarajiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwezi Machi 2024.

“Kama mnavyoona hii ni oparesheni inayofanywa na Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) hususan Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo ujenzi huu unahusisha sekta nyingi na ndio maana nimeongozana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleeo ya Makazi na sekta nyingine za Nishati na Maji ili kufanya haraka kwa wakazi hawa kupata Malazi ya kudumu,” ” amesema Dk. Tax

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Geophrey Pinda amesema Wizara yake ndio ya mwanzo kabisa katika utekelezaji wa mradi huu kwani ndio inafanya maandalizi ya kupanga na kupima ardhi ili sekta nyingine zianze kufanya kazi kikamilifu.

“Wizara yetu ndio ya kwanza kabisa kufika eneo hili kuja ambapo ilikuja kulitambua eneo hili la msomera tangu lilipotolewa agizo la kuwaandalia makazi wananchi wa eneo hili, hivyo tumefanikiwa kulipanga na kulipima japo bado baadhi ya maeneo tunaendelea kuyapanga na kutatua migogoro ya mipaka,” alisema Pinda.

Pinda amesisitiza kwamba wizara yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na taasisi nyingine katika kuharakisha ukamilishaji wa operesheni hiyo.

Katika kukamilisha kazi hii Pinda ameahidi kukutana na viongozi wa Wilaya ya Simanjiro na Kilindi wenye mgogoro wa mipaka ya Wilaya na Wilaya ili kutatua mgogoro huo unaokwamisha zoezi la kupanga makazi ya wananchi hao.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here