Home BIASHARA Serikali kutumia muundo wa NMB umiliki wa mashirika ya umma

Serikali kutumia muundo wa NMB umiliki wa mashirika ya umma

Google search engine
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (kushoto), akipokea Waraka wa Matarajio ya Program ya Utoaji wa Hati Fungani ya Muda wa Kati (MTN) kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, wakati wa uzinduzi wa NMB Jamii Bond jijini Dar es Salaam jana. (Na Mpiga Picha).

Serikali kutumia muundo wa NMB umiliki wa mashirika ya umma

Na Mwandishi Wetu

Kutokana na mafanikio makubwa iliyonayo Benki ya NMB, Serikali imesema inapanga kuutumia muundo wa umiliki wake kuchagiza tija katika kuyaendesha mashirika ya umma ili yawe na faida stahiki kwa taifa.

Hiyo ni kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, ambaye amekiri na kusema kuwa serikali inafurahishwa na ufanisi wa benki hiyo  kiutendaji.

“Hatujutii kabisa kuwekeza katika taasisi hii kutokana na inavyoendelea kufanya vizuri na ni mfano wa kuigwa kwa mashirika yetu tunapoelekea kupunguza utegemezi wake kwa serikali katika kujiendesha,” amesema Mchechu Jumatatu, wiki hii jijini Dar es Salaam.

“Katika mageuzi tunayoyafanya kuyarekebisha mashirika yetu tunataka umiliki wake kuwa kama wa NMB ambao umekuwa na mafanikio makubwa kiuendeshaji na kiutendaji,” kiongozi huyo alibainisha kwenye hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa hatifungani mpya ya NMB Jamii Bond,” amesemaMchechu aliongeza kuwa Serikali haitaki tena mashirika yake yaendelee kutegemea fedha za kujiendesha na mitaji kutoka kwake bali yawe na utaratibu kama wa NMB wa kuyatumia masoko ya mitaji na dhamana kwa ajili hiyo.

Benki hiyo ambayo wamiliki wake wakubwa ni Serikali yenye asilimia 31.8 ya hisa zote na Arise BV yenye asilimia 34.9, imeweka sokoni dhamana ya NMB Jamii Bond kutafuta TZS bilioni 75 na ziada ya TZS bilioni 25 kutoka kwa wawekezaji itakaowalipa riba ya asilimia 9.5.

Hatifungani hii ambayo ni toleo la kwanza la Waraka wa Matarajio wa Programu ya Utoaji wa Hatifungani ya Muda wa Kati (MTN) wenye thamani ya jumla ya TZS trilioni moja pia ina kipengele cha kukusanya dola za Kimarekani milioni kumi (US$10 million)  na nyongeza ya US$5 kama yatakuwepo mahitaji yake zaidi.

Wamiliki wake wengine ni pamoja na wawekezaji wadogo wenye jumla ya hisa asilimia 22.4 na wananchi wa kawaida ambao jumla ya hisa zao ni asilimia 10.9.

Kwa mujibu wa Mchechu, umiliki wa aina hii ndiyo unaotoa taswira na maana halisi ya umma kumiliki mashirika tofauti na ilivyo sasa ambapo hilo linafanyika kupitia serikali.

“Muundo huu wa umiliki unaoihusisha Serikali, wawekezaji wa kimkakati na wananchi ndiyo utakaotumika katika uendeshaji wa mashirika mengi kwani tayari tunaona faida zake kupitia NMB.”

Faida hizo ni pamoja na kuongoza kwa faida ambapo NMB ni ya tatu miongoni mwa benki za Afrika Mashariki huku ikiwa moja ya benki zenye ufanisi mkubwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa gharama na mapato (CIR).

Aidha, mbali na kuwa mlipaji mkubwa wa kodi, gawio lake kwa Serikali limekuwa likiongezeka kila mwaka na kufikia jumla ya Sh bilioni 113 kati ya 2019 na 2022. NMB pia ni mdau mkubwa wa serikali katika kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo na ustawi wa jamii.

Kutokana na kuwa mzigo mkubwa kwake, Serikali ya Awamu ya Sita imetangaza kuyafanyia mageuzi makubwa mashirika yake 248 inayoyamiliki kwa asilimia 100 ili yawe na tija stahiki katika maendeleo na mchango kama wa NMB katika ujenzi wa taifa.

Mchechu ameipongeza NMB kwa kuja na Hatifungani ya Jamii ambayo Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna, amesema ni kwanza Afrika Mashariki kuzingatia kwa pamoja masuala ya kijani na ustawi wa jamii.

“Hatifungani ya Jamii ya NMB ni kitu kizuri kwani si tu ni fursa kwa wawekezaji na maendeleo, lakini pia italichangamsha soko la hisa na tunaenda kuyaruhusu mashirika yetu kuanza kuvitumia vyanzo vya mapato kama hivi,” Mchechu alisisitiza na kusema mageuzi yanayofanywa na Serikali yanastahili kuungwa mkono.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi na shirikishi sokoni huku akitoa rai kwa mashirika ya umma kutumia fursa hii kupata fedha za kujiendeleza.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here