Home KITAIFA DC SAME AMUONYA MWEKEZAJI ANAYEDAIWA KUZUA TAHARUKI

DC SAME AMUONYA MWEKEZAJI ANAYEDAIWA KUZUA TAHARUKI

Google search engine

*Amtaka kutoichonganisha Serikali na wananchi, mwenyewe atoa neno

Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, akizungumza na wananchi
Wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya (hayupo pichani)
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni akikagua shamba linalodaiwa kuibuka mgogoro baina ya wananchi na mwekezaji

Na MWANDISHI WETU

-SAME

Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ametoa onyo kwa mwekezaji wa Kampuni ya LM Investment inayozalisha Katani wilayani hapa kwa kumtaka afute utaratibu.

Hatua hiyo inatokana na kuibuka kwa mjadala mitandaoni ambao unaelezwa kuzua taharuki ikiwamo kuwashutumu wanakijiji wa Kata ya Maore Wilaya ya Same, kudaiwa kuvamia shamba lake ya mikonge.

Akizungumza leo Septemba 11, 2023  na wananchi wa vijiji vya Mpirani, Msufini na Ndungu, DC Kasilda, amemtaka mwekezaji huyo kuacha kusambaza mitandaoni taarifa ambazo si sahihi na zenye lengo la kuzua taharuki kwa kutaka kuichonganisha Serikalin a wananchi jambo ambalo linaweza kuharibu taswira ya usalama wilayani hapa.

Amesema lengo la Serikali kutatua kero na changamoto za wananchi wanyonge pamoja na kutafuta suluhu hasa kwa wawekezaji pindi inapotokea sintofahamu miongoni mwa jamii.

“Mimi nitumie mkutano huu kumuonya mwekezaji juu ya vitendo vyake vya kuzua taharuki kwa kudanganya Watanzania kwamba wananchi wa Ndungu, Msufini na Mpirani wanavamia maeneo yake na kuchoma Mkonge. Ninatoa onyo hili aache mara moja pindi akirudia Serikali haitamwacha tutamchukulia hatua za kisheria kwa sababu anaichonganisha Serikali na wananchi,” amesema Mgeni

Kutokana na hali hiyo DC Mgeni, amewataka wanakijiji wa Kata ya Maore wawe na uhusiano mzuri na mwekezaji huyo kama njia ya kuharakisha maendeleo yenye tija kati ya mwekezaji na wanakijiiji huku akiwataka kuhakisha zoezi la malipo ya ankara ya umilikishwaji wa viwanja hekta 300 walizopewa na serikali y yanafanyika mapema.

DC Mgeni, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Same kukamilisha ndani ya wiki moja  zoezi la uwekaji wa alama za mipaka mikubwa itakayotenganisha eneo la mwekezaji na la Kijiji ili mwekezaji asipate sababu nyingine ya kuzusha taarifa za uongo kama alizozizusha hapo awali.

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Maore, Abedi Ally amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuwapa matumaini wanakijiji hao kwamba ardhi hiyo ni mali yao si ya mwekezaji huku akiwasisitiza wanakijiiji ambao bado hawajalipia viwanja vyao wavilipie mapema ili zoezi la kukabidhi maeneo hayo lifanyike mapema wiki ijayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kata ya Maore, Rajabu Kijangwa na Yasin Hassan wameshukuru Mkuu wa Wilaya kuliingilia kati jambo hilo ambalo limekuwa likiwanyima furaha kutokana na tabia ya mwekezaji huo ambaye amekuwa akisafisha shamba lake kwa kuchoma nyasi Kisha kurekodi video na kuisambaza mtandaoni na kudai kuvamiwa kwa shamba lake.

Kutokana na hali hiyo mwandishi wa Habari hizi, alimtafuta Mwekezaji huyo, Omari Mndeme  ambapo amesema kuwa wanakijiji wa kata hiyo wamemdanganya Mkuu wa Wilaya kuwa hakuna eneo lililochomwa wala kukatwa mikonge .

Amesema shamba hilo lina ukubwa wa takribani hekari  mbili ambazo zimechomwa na kukatwa mikonge na wanakijiji hao ambapo amesema kuna wakati amekuwa akitishiwa na mapanga.

“Mimi nimeamua katika kuhakikisha najilinda na vitisho hivi nimeandika barua kwa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Ardhi ambapo anategemea kujibiwa hivi karibuni,” amesema Mndeme

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Georfrey Pinda alifika katika Kijiji hicho ambapo aliwakabidhi  rasmi hekari 300 kwa wananchi ambapo kila kijiji kiligawiwa hekari 100 ambapo alimtaka mwekezaji huyo kutowabughudhi wananchi hao  kwani ardhi hiyo wamepewa na Rais Samia Suluhu Hassan na imekuwa mali yao.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here