Na Farida Ramadhani, WF
– Dar es Salaam
Wananchi wamekaribishwa kutembelea banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam, ili kupata elimu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na Wizara hiyo pamoja na baadhi ya taasisi zilizo chini yake.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Jenifa Omolo alipotembela banda hilo na kuzungumza na waoneshaji kutoka Wizara na Taasisi zake.
Alisema katika banda hilo wananchi watapata elimu kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali na uandaaji wake, sera mbalimbali za usimamizi wa kodi, usimamizi wa mali za Serikali, mifumo ya malipo na mishahara.
“Kuna taasisi za elimu ambazo zinawawezesha wahitimu kujitegemea baada ya kumaliza masomo yao lakini pia kuna taasisi za fedha na zinazojihusisha na uwekezaji”, alibainisha Omolo.
Alisema banda hilo linatoa elimu ambayo itamuwezesha mwananchi kujua namna Serikali inavyopanga mipango mbalimbali ya maendeleo, inavyosimamia miradi ya maendeleo pamoja na ujenzi wa miundombinu.
Omolo alibainisha kuwa wananchi watapata elimu kuhusu mifumo mbalimbali iliyoanzishwa na Serikali kwa ajili ya kusimamia fedha na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yake.
Kwa upande wa baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo waliipongeza Serikali kwa kuweka maonesho hayo ambayo yamewaezesha kujua mambo mbalimbali yanaotekelezwa na Serikali hususani masuala ya usimamizi wa fedha na kukuza uchumi.
Wameshauri elimu hiyo iwe endelevu hata baada ya kumaliza maonesho hayo kwa kuwa wananchi wengi bado hawanauelewa wa mambo mengi yanayotekelezwa na Serikali.