Home KITAIFA Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar awataka wahariri kuzuia dosari kwenye...

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar awataka wahariri kuzuia dosari kwenye matumizi ya Kiswahili

Google search engine
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, akizungumza na wahiriri wa vyombo vya habari nchini habari kuelekea maadhimisho ya siku ya Kishwahili duniani, uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Mjini Unguja.
W

Na Mwandishi Wetu

– Zanzibar

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, amewataka wahiriri wakuu wa vyombo vya habari nchini kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia dosari katika matumizi ya Kiswahili kwa kujua au kutojua.

Amesema licha ya juhudi zinazofanywa na wahariri katika kutumia Kiswahili fasaha, lakini bado wapo waandishi wa habari wachache wamekuwa wakiitia dosari lugha hiyo ama kwa kujua au kutia mbwembwe zao.

Makamu wa Pili ameyasema hayo  katika mkutano wa wahariri wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari kuelekea maadhimisho ya siku ya Kishwahili duniani, uliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Mjini Unguja.

Amesema kuwa, ipo haja kwa wahriri kuzingatia matumizi sahihi ya Kiswahili katika kazi zao za kila siku kwani ni sehemu ya kuitangaza zaidi lugha hiyo duniani.

“Dhamana mliyoibeba kuhusu kugha ya Kiswahili ni kubwa na hapana shaka kuwa nyinyi ni walimu wa lugha hii kutokana na majukumu yenu,” amesema.

Hivyo alieleza kuwa, bila shaka mkutano huo utasaidia kuleta mjadala wa kina katika mustakabali wa lugha na mambo mengine ya tasnia ya habari.

Alieleza kuwa kwa kuzingatia hayo yote, jukumu la kukiendeleza Kiswahili liko mikononi mwa wahariri hao na kuamini kuwa wataendelea kuikuza lugha hiyo ndani na nje ya nchi itumike katika vikao na majukwaa ya kimataifa.

Aidha, aliyapongeza mabaraza ya Kiswahili BAKITA na BAKIZA kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia matumizi na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.

Amesemasema kuwa, anafahamu BAKIZA imesambaza kamusi ya Kiswahili katika vyombo vya habari Zanzibar kwa lengo la kuwasaidia wahariri kurejelea misamiati sahihi pale ambapo kuna shaka ya usahihi katika kutoa habari.

Aidha, alisema serikali inawahamasisha watu wote wenye ujuzi na maarifa yanayoendana na lugha ya Kiswahili kuchangamkia fursa zilizopo duniani kote.

Akitaja fursa hizo, alisema ni pamoja na ukalimani, tafsiri, uhariri, uandishi, utangazaji wa habari na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni.

“Natambua kuwa kupitia mabaraza yetu ya lugha BAKITA na BAKIZA, Kiswahili kimesambaa na kuwekewa mikakati katika nchi za Ujerumani, Uholanzi, Italia, Nigeria, Nchi za Falme za Kiarabu, Malawi, Rwanda na Zimbabwe,” amesema.

Alieleza kuwa, huo ni mwanzo mzuri katika kuitangaza na kuinadi lugha ya Kiswahili kutafuta manufaa zaidi na kuyataka mabaraza hayo kuendeleza juhudi hizo walizozianzisha.

Hivyo alitumia nafasi hiyo kuwataka kutumia jukwaa hilo kutafuta fursa za utangazaji katika vyombo vya habari vya kimataifa ambapo hadi sasa zipo redio na vituo vya televisheni za nje ya nchi zipatazo 30 zinazorusha matangazo yake kwa lugha ya kiswahili.

“Jukwaa lenu liwe mfano katika kuangalia fursa hizo na kuwaunganisha wataalamu wa tasnia ya habari,” amesema.

Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani kwa mwaka huu inayosema ‘Kiswahili chetu ni umoja wetu’ alitoa wito kwa jukwaa hilo kushirikiana na mabaraza katika kuzungumza Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari.

Hemed amesema kuwa serikali katika kuimarisha sekta ya habari inaifanyia marekebisho sheria ya habari iendane na mabadiliko yanayojitokeza katika sekta ya mawasiliano ya habari na teknolojia.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amesema, Wizara zote mbili zinamkakati wa kuendelea kukifanya kiswahili kuwa bidhaa na kwamba kiendelee kuwafaidisha watazania kwa kufanya mambo mbalimbali.

Akiyataja mambo hayo amesema kama vile kupeleka walimu nje ya Tanzania kufundisha kiswahili lakini kupokea wageni mbalimbali ambao wanaingia katika vyuoni Tanzania kujifunza ligha ya kiswahili.

Amesema, Wizara huzungumza na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi kueneza kiswahili katika nchi wanazoziwakisha sambamba na kuwapelekea kamusi za kiswahili na vitabu mbali mbali ambavyo zinaonyesha matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili.

Lakini pia alisema, wanaendelea na mkakati wa kuhamasisha matumizi bora ya kiswahili kwa kutumia mabaraza ya kiswahili BAKITA na BAKIZA.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Khamis Mwinjuma amewataka wahariri kuweka namna bora ya kutumia fursa zinazopatikana kwenye kiswahili kwa ajili ya kukiendeleza.

“Jambo hilo si kwamba litawasaidia nyinyi tu lakini litaisaidia nchi kwa ujumla na ile dhana ya kwamba sisi ndo wenye kiswahili haswa inatakiwa kuendelea kubaki,” amesema.

Amesema, serikali zote mbili zinafanya mambo mengi sana ya kuhakikisha kwamba lugha ya kiswahili inakuwa ni miongoni mwa nembo za taifa.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here