Home KITAIFA WAKURUGENZI WAPEWA SAA 48 KUPELEKA BENKI BILIONI 2.4 ILIYOKUSANYWA KUPITIA POS

WAKURUGENZI WAPEWA SAA 48 KUPELEKA BENKI BILIONI 2.4 ILIYOKUSANYWA KUPITIA POS

Google search engine
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Mitaa, Deo Ndejembi

NA MWANDISHI WETU

-DODOMA

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Deo Ndejembi, amewagiza Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimekusanya mapato kupitia mfumo mpya wa TAUSI na hawajapeleka fedha benki kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa ndani ya siku mbili ifikapo tarehe 30 Juni 2023 kabla ya mwaka wa fedha 2022/23 kuisha.

Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo tarehe 28, Juni 2023 katika Kikao na Idara ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya kupokea taarifa ya hali ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha katika Halmashauri zote nchini.

Ndejembi amesema kufikia tarehe 25 Juni 2023 kiasi cha Sh bilioni 2.4 zilizokusanywa kupitia POS katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa TAUSI katika halmashauri zilikuwa hazijapelekwa benki lakini kwenye mfumo zinaonekana zimekusanywa.

“Wakati napitia taarifa nimeona bilioni 2.4 ambayo inaonekana kwenye mfumo imekusanywa lakini haijapelekwa benki, sasa niwatake Wakurugenzi wote wa maeneo ambayo fedha imeonekana kwenye mfumo imekusanywa lakini haijapelekwa benki, kupeleka fedha hizo benki ndani ya siku mbili hizi kabla owaka wa fedha kuisha”

Aidha, Ndejembi ameziagiza Halmashauri 103 ambazo hazijafanya usuluhishi wa Kibenki (Bank Reconciliation) ambao unatakiwa kufanyika ndani ya siku 15 baada ya mwezi kuisha kuhakikisha wanafanya usuluhishi wa Kibenki ndani ya siku mbili ili kuepuka hoja za CAG.

Ndejembi amesema Mkurugenzi yeyote atakayeshindwa kutekeleza maagizo hayo ndani ya Siku mbili kabla ya mwaka wa fedha kuisha atoe maelezo kwa maandishi Kwanini hajatekeleza na Kwanini asichukuliwe hatua kali.

Kadhalika, Ndejembi amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote zinazikusanywa katika Halmashauri kuanzia ngazi ya vijiji, mitaa, kata na huduma za Afya na Elimu kuingizwa kwenye mfumo ili kuongeza ufuatiliaji wa fedha hiyo.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here