Home KITAIFA Jaji Mwangesi: Ukosefu wa Maadili viongozi wa umma ni kilio

Jaji Mwangesi: Ukosefu wa Maadili viongozi wa umma ni kilio

Google search engine
Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Sivangilwa Mwangesi akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Wahariri wa Vyombo vya Habari uliofanyika leo June 17, 2023 Jijini Dar es Salaam
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi katika mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Emma Gelani, akitoa mada iliyohusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika mkutano huo.
Katibu Idara ya Ukuzaji Maadili, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Waziri Kipacha, akitoa mada iliyohusu Ukuzaji wa Maadili katika mkutano huo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Honoratus Ishengoma, akitoa ukaribisho kwa wahariri wa Vyombo vya habari katika Mkutano wa Sekretarieti hiyo na Wahariri uliofanyika leo Juni 17, 2023 Dar es Salaam.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Anitha Mendoza akifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika Mkutano huo.

Na Mwandishi Wetu

-Dar es Salaam

KAMISHNA wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangilwa Mwangesi amesema ukosefu wa maadili kwa sasa umezua kilio kila kona hapa nchini kuanzia watoto wadogo wa shule hadi viongozi wa umma na kuwataka wadau wote kushirikiana kukabiliana nalo.

Jaji Mwangesi ameyasema hayo Juni 17, 2023 mkoani Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari nchini ulioratibiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu kuelimishana na kujadili mambo muhimu kuhusu ofisi hiyo.

“Hakuna ubishi katika ukweli kwamba suala la ukosefu wa maadili limezua kilio katika kila kona ya nchi yetu, kuanzia watoto wadogo wa shule, vijana hadi viongozi ambao sisi ndio wanaotuhusu, suala la uadilifu ni suala adimu, tunaamini hili sio wadao wote tukishirikiana tutakabiliana nalo, sio letu pekee,” amesema Jaji Mwangesi.

Amesema maadili yanasimamiwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 pamoja na kanuni zake na kuwaomba wahariri wasaidie kuelimisha jamii misingi ya maadili na ili kuwa na viongozi bora.

Kutokana na hali hiyo Jaji Mwangesi amesema tasnia ya habari ndio jicho, sikio na mdomo wa jamii na kwamba majukumu ya taasisi hiyo yakieleweka vizuri kwa wanahabari watachakata vyema taarifa zinazowafikia kuhusu viongozi wa umma na wananchi wengine kwa kuzihoji, kudadisi na kuzipembua kwa mujibu wa sheria.

Amesema vyombo vya habari na taasisi hiyo wakishirikiana katika mapambano ya utovu wa maadili katika jamii yatasaidia kurekebisha mienendo ya watu na kupunguza tatizo hilo.

Akitoa mada kuhusu Ukuzaji Maadili, Katibu wa Idara ya Ukuzaji wa Maadili wa sekretarieti hiyo, Waziri Kipacha amewataka wahariri kuwa waadilifu ili wapate ujasiri wa kuelimisha jamii kuwa na maadili.

“Ili tuwe mfano kwa wengine na sisi tuwe waadilifu, mfano tukifichua mambo yanayofanywa isivyo halali na watumishi wa umma na sisi tuhakikishe ni wasafi ili jamii inaposoma habari hizo isihoji maswali ya uadilifu wako,” amesema Kipacha.

Amesema maendeleo ya sasa duniani yakiwemo ya teknolojia na utandawazi yamesababisha jamii kuwa na mwingiliano mkubwa wa mila, tamaduni na kuitaka jamii ya Kitanzania kuendelea kutunza tamaduni zao na kuacha kuiga za kigeni ambazo hazina misingi mizuri ya maadili.

Kutokana na hali hiyo,  amewataka wananchi kutoa taarifa za mienendo mibaya kwa viongozi pindi wawaonapo wakifanya katika jamii na kwamba sheria inamlinda mtoa taarifa hivyo wasiogope.

Kuhusu kiwango cha maadili cha sasa kwa viongozi wa umma, taasisi hiyo imesema bado utafiti wa karibuni haujafanywa ili kuja na takwimu halisi lakini kwa utafiti wa mwaka 2016, ulionesha kiwango cha maadili kwa kundi hilo kiko asilimia 50.

Hata hivyo, wamesema wako kwenye mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya  kufanya utafiti kuhusu kiwango cha maadili kwa viongozi wa umma nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema mkutano huo umekuwa jambo jema kwa sababu unawaleta pamoja na taasisi hiyo na vyombo vya habari na kuona jinsi ya kushirikiana katika kujenga misingi ya maadili kwa jamii.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here