Home BIASHARA NMB yachangia vifaa vya milioni 10/= kusaidia wajawazito Wilayani Korogwe

NMB yachangia vifaa vya milioni 10/= kusaidia wajawazito Wilayani Korogwe

Google search engine
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo (kulia) akimkabidhi mwanawake mjamazito moja ya msaada wa vifaa vya kujifungulia vilivyotolewa na benki ya NMB venye thamani ya shilingi milioni 10. kushoto ni Kaimu meneja wa kanda ya Kaskazini wa Benki ya NMB, Praygod Mphuru.

Na Mwandishi Wetu

-Korogwe

Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa vya kujifungulia kwa kina mama wajawazito zaidi ya 500 katika kituo cha afya cha Mombo kilichopo Wilayani Korogwe Mkoani Tanga vyenye thamani ya shilingi milioni 10 vinavyokwenda kuwatatulia changamoto ya vifaa wakati wa kujifungua. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo vya kujifungulia kwa kina mama hao, Kaimu Meneja wa benki ya NMB kanda ya Kaskazini Praygod Mphuru amesema kuwa afya ni moja ya kipaumbele chao kwani  ni msingi mkubwa kwa maendeleo ya Taifa lolote duniani. 

Meneja huyo wa kanda amesema kuwa vifaa hivyo walivyokabidhi ni moja ya ushiriki wao katika maendeleo ya jamii hivyo wanao wajibu wa kuhakikisha jamii inayowazunguka inafaidika kutokana na faida wanayoipata. 

“Tulipopata maombi haya ya kuchangia maendeleo ya afya katika wilaya ya Korogwe tulifarijika na kuamua mara moja  kuja kushirikiana nanyi ili kuwa chachu ya maendeleo ya sekta hii muhimu kwa jamii yetu na hasa katika wilaya hii ya korogwe na hususani katika hospotali hii ya Halmashauri ya mji ya Mombo, alisema Meneja Mphuru. 

Aidha alisema kwa miaka kadhaa sasa Benki hiyo imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu (madawati na vifaa vya kuezekea)  afya (vitanda,  magodoro yake na vifaa vingine vya kusaidia matibabu)  pamoja na kusaidia majanga yanayoipata nchi. 

“Tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka kwahiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wetu ni kwa zaidi ya miaka 7 mfululizo tumekuwa tukitenga asilimia 1% ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka, “alisistiza Kaimu meneja huyo wa kanda kaskazini. 

Awali akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo kwa kinamama wajawazito hao,  Mkuu wa wilaya Korogwe Jokate Mwegelo amewapongeza benki ya NMB kwa msaada huo na kuvitaka vituo vyote vya afya na zanahati na hospitali ya wilaya Korogwe kutoa huduma za afya kwa watu kwa kuzingatia utu na huruma. 

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa kina mama wengi walikuwa na uhitaji na msaada huo hivyo msaada huo unakwenda kujibu agenda ya maendeleo endelevu duniani na kwamba huduma ya afya ni muhimu kuwafikia watu wote kuanzia ngazi ya msingi. 

“Tikizungumzia ngazi ya msingi ni kwamba mama anaweza kuwa anataka kujifungua wakati wowote sasa kama kuna mtoa huduma ngazi ya jamii halafu mama ana hivi vifaa anaweza kumuhudumia yule mama tayari tunakuwa tumerahisisha upatikanaji wa huduma ya afya, “alibainisha DC Jokate .

Sambamba na hayo DC Jokate amesema msaada uliotolewa kituoni hapo unakwenda kuwasaidia kina mama wajawazito zaidi ya 140 mpaka 150 wanaokwenda kujifungua kituoni hapo kwa kila mwezi hivyo ni eneo linalohudumia wananchi wengi ambapo amesisitiza kituo hicho kutazamwa kwa jicho la tatu. 

“Matamanio yangu huko mbeleni kituo hiki kipande hadhi na kiitwe hospitali ya wilaya najua inawezekana sababu serikali ya awamu ya sita imejikita kwenye kuboresha miundombinu kwenye sekta ya afya niwaambie ndugu zangu Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan yupo kazini anawapenda na anawajali lakini pia anawaangalia kwa jicho la kipekee, “alisema DC Jokate. 

Kwa upande wake mganga mfawidhi wa kituo cha afya cha Mombo Dkt John Mapoli amesema kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuwasaidia kinamama hao kujifungua katika mazingira salama kwani kina mama hao wakati mwingine hufika kituoni hapo wakiwa hawana vifaa vya kujifungulia. 

“Kwa kweli NMB tunawashukuru sana wamekuwa jirani na sisi na wamekuwa msaada kwa vitu vingi tunafurahi sana leo hii kupokea vifaa hivi vya kujifungulia wamama zaidi ya paki 500 za kujifungulia, “alisema Dkt John

Baadhi ya kina mama wajawazito waliokabidhiwa vifaa hivyo wameishukuru benki ya NMB na kueleza kuwa msaada huo umekuwa ni neema kwao kwani umekuja kwa wakati sahihi. 

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here