Na Mwandishi Wetu
-DODOMA
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu ameitaka Serikali kuangalia upya gharama za vipimo kwenye hospitali za Serikali ambazo zinalingana na hospitali binafsi ambazo zinalingana na hospitali binafsi wakati Serikali inatoa mishahara, mitambo na umeme.
Hhayo ameyasema leo Mei 12, 2023 baada ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2023/24.
“Pamoja na kazi nzuri mnazozifanya jaribuni kupitia upya gharama za vipimo katika hospitali za Serikali. Mishahara, umeme analipa Rais, mitambo ananunua Rais hakuna sababu ngoma iwe droo huku serikalini na huku uraiani,”amesema.
Amesema wastaafu, wazee, wanawake uwezo wa kwenda kupima vipimo hivyo ni kazi sana na kwamba wakitazama Mfuko wa Bima ya Afya unaathirika kwa sababu ni lazima ulipe gharama kubwa za vipimo.
“Kuna nchi kama India kusafisha damu ni Dola za kimarekani 28 (sawa na Sh65,000) tu pamoja na vifaa vyake. Kwa hiyo jaribuni kwenda kutazama ili kupunguza gharama kumsaidia Rais ili wananchi wake waweze kuwa na mapenzi zaidi,”amesema.