Home KITAIFA Mchakato wa Katiba Mpya sasa waanza kuiva, Rais Dk. Samia atoa maagizo

Mchakato wa Katiba Mpya sasa waanza kuiva, Rais Dk. Samia atoa maagizo

Google search engine
Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza kikao cha viongozi mbalimbali wa Serikali kinachohusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya, kilichofanyika Jumamosi Mei 6, 2023 Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma. Picha na Ikulu

Na Mwandishi Wetu

-Dar es Salaam

Mchakato wa Katiba Mpya sasa umeiva. Ndivyo unaweza kusema hasa baada ya siku chache Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro kutangaza kwa umma juu ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya uliokwama, ambapo sasa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuitisha kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa.

Lengo la kuitishwa kwa Baraza hilo linaloshirikisha vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu mbalimbali kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Kikosi kazi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti, Profesa Rwekaza Mukandala pamoja na mambo mengine, kilipendekeza mchakato wa Katiba uliokwama mwaka 2014 kwa hatua ya Katiba Pendekezwa kufufuliwa.

Rais Samia ametoa maagizo hayo Jumamosi Machi 6, 2023, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma alipofanya kikao na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Jaji Mutungi na Waziri Ndumbaro.

Maagizo hayo ameyatoa ikiwa ni wiki chache zimepita tangu Waziri Ndumbaro awasilishe Bajeti ya Wizara yake ya Katiba na Sheria Bungeni na kupitishwa ikiwa na vipaumbele mbalimbali na kipaumbele cha kwanza ni mchakato wa Katiba mpya.

Pia, vipaumbele vingine ni maboresho ya sheria za uchaguzi kuelekea chaguzi zijazo mwaka 2024 wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025 wa madiwani, ubunge na Urais.

Katika kikao cha Rais Samia na viongozi hao wa Serikali, kimejadili ushirikishwaji wa wadau mbalimbali na hasa wananchi kwenye mchakato huo wa Katiba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, imesema mbali ya mchakato wa Katiba, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni  marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi, zikiwemo sheria za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa vyama vya Siasa.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama na Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here