Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Jokate Mwegelo amefanya ziara katika Bandari ya Tanga akiwa na Wafanyabiashara, Viongozi , Wakulima na Wadau wengine wa Korogwe ambapo amesema lengo ni kujionea maboresho ya Bandari hiyo yaliyotumia zaidi ya Sh.bilioni 400 na kuwapa chachu wana Korogwe kusafirisha bidhaa zote Tanga badala ya kutegemea Bandari ya Dar es salaam pekee.
Akizungumza leo Mei 6,2023 bandarini hapo Jokate amesema uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Dk.Samia Suluhu Hassan ambapo zaidi ya Sh.bilioni 400 zimetumika kufanya maboresho ya Bandari ya Tanga .
“Mmeona Meli hii kubwa huko nyuma ilikuwa haiwezi kufika, tumekuja wafanyabiashara na lazima tukubaliane tani tunazozalisha wote tusafirishe hapa.Tukubaliane na Wakala wa Meli ili wapunguze tozo zao lakini apunguze lazima awe na uhakika wa kuondoa kontena kadhaa, malengo yetu ni kwamba bidhaa zote zinazozalishwa Wilayani Korogwe tutumie Bandari ya Tanga, ili fedha nyingi zilizowekezwa hapa ziwe na tija,”amesema Jokate.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema “Kwa harakaharaka kuanzia Januari hadi Machi ,2023 tumekusanya zaidi ya Sh. Bilioni 7, maendeleo kwa Bandari ya Tanga baada ya uwekezaji wa Bilioni 429.1 maendeleo ni makubwa, kwa mwaka tulikuwa tunazalisha tani Laki 7.5 lakini baada ya maboresho tunazalisha mpaka tani Mil 3, meli kubwa sasa zinaingia moja kwa moja”