Home MAKALA Ufugaji bora wa Jongoo Bahari ni mlango wa kuinua uchumi wa Buluu...

Ufugaji bora wa Jongoo Bahari ni mlango wa kuinua uchumi wa Buluu Tanzania

Google search engine

Na Victor E. KAIZA.

(Victor E. Kaiza ni Mkufunzi na Mtaalam wa Ukuzaji viumbe maji wa Wakala wa Elimu na Mifugo na Uvuvi, Kampasi ya Mikindani – Mtwara, Tanzania – 0715 900 425)

Jongoo bahari ni mnyama gani

Jongoo bahari ni miongoni mwa wanyama wa baharini wasio na uti wa mgongo ‘invertebrates’ jamii ya wanyama wenye ngozi laini yenye miiba kitaalam huitwa ‘echinoderms’. Jongoo bahari ni wanyama wenye ngozi laini yenye miiba wanaopenda kuishi chini ya bahari. Makazi ya asili ya jongoo bahari ni maeneo yenye miamba, mchanga au tope kulingana na aina ya jongoo bahari. Kibaiolojia, jongoo bahari ni mnyama asiye kuwa na macho, ubongo wala moyo. Mfumo wake wa kujongea hutumia misuli milaini iliyopo kwenye tumbo lake iitwayo ‘podia’.

Pia, jongoo bahari ana mfumo wa kula chakula kwa kutumia mikono midogo izungukayo mdomo wake iitwayo ‘feeding tentacles’. Chakula kikuu cha jongoo bahari ni mabaki ya kiorganiki yatokanayo na kuoza kwa viumbe-hai yatuamayo kwenye udongo, miamba ya bahari, nyasi bahari na mwani. Jongoo bahari hula kwa kubugia udongo wenye mabaki hayo kisha kuuchuja na kuutoa ukiwa msafi kwa njia ya haja kubwa. Hivyo ulaji huu wa jongoo bahari huboresha mazingira ya bahari kwa kulainisha udongo wa bahari na kupunguza mrundikano wa takataka laini za kiorganiki baharini. Hivyo, uwepo wa jongoo bahari una faida kwenye mazingira ya bahari kwani kunasaidia bahari kujisafisha yenyewe.

Matumizi ya jongoo bahari.

Jongoo bahari wana matumizi mengi kwa binadamu kwani hutumika kama chakula au tiba. Kihistoria matumizi ya jongoo bahari kama chakula na tiba yalianza kurekodiwa kipindi cha Tawala za Ming (Ming dynasty) karne ya 13 hadi ya 17 B. K. nchini China. Jongoo bahari hutumika kwa ajili ya chakula, lishe-tiba na tiba za dawa za kichina na dawa za kifamasia. Jongoo bahari hupikwa kama supu au hukaangwa na viungo kisha huliwa kama chakula cha binadamu. Jongoo bahari hutumiwa na jamii za waAsia wengi kutibu magonjwa ya upungufu wa nguvu za kiume, uchovu wa mwili na maumivu ya viungo yaani arthritis. Kifamasia, jongoo bahari hutoa viambata ambavyo hutumika kutibu magonjwa ya bakteria, virusi, malaria na kansa. Pia, baadhi ya viambata hutumika kutengenezea vipodozi vya kuimarisha afya ya ngozi.

Hivyo, jongoo bahari ameongezeka matumizi na nchi kama Marekani hununua jongoo bahari kwa ajili ya kutengeneza madawa ya kifamasia ya kutibu magonjwa. Pia, kuna baadhi ya viambata ambavyo hutumika katika maabara za kisayansi za chembehai za vinasaba yaani DNA na RNA. Hata nchini Tanzania, kuna baadhi ya hoteli unaweza kuagiza sahani ya jongoo bahari aliyepikwa vizuri. Maoni ya wengi walibahatika kuonja jongoo bahari aliyepikwa husema kuwa ana ladha kama ya ngisi ila yenye chumvi na ukakasi.

Biashara ya jongoo bahari duniani.

Kwa sasa, biashara ya jongoo bahari inaendelea duniani, kwa mujibu wa takwimu za FAO, uzalishaji wa jongoo bahari duniani unakadiriwa kuwa tani 250,000 ambazo tani 50,000 zinatokana na uvuvi wa jongoo bahari na tani 200,000 unatokana na ufugaji wa jongoo bahari. Aina mbalimbali za jongoo bahari kama, Jongoo maji/Myeupe au ‘sandfish’ kwa kingereza (Holothuria scabra), pauni (Holothuria nobilis), barangu (Holothuria fuscogilva), spinyo baba (Thelenota ananas), spinyo mama (Spichopus hermanni), spinyo za kijapani (Apostichopus japonicus), jongoo bahari za Mediterania (Holothuria tubulosa na Holothuria mammata), jongoo bahari za marekani (Cucumaria frondosa) ni jongoo zenye soko kubwa sana nchi za Uchina, Japani, Korea kusini, Thailand na Marekani. Kwani bei zake hutegemeana na madaraja pale zikiwa kavu na huweza kufika shilingi millioni 2.5 hadi laki 5 ya kitanzania kwa kilo moja.

Jongoo bahari aina za mbura (Actinopyga miliaris), Mbura khaki (Actinopyga mauritania), kichupa (Holothuria atra) na nyinginezo ni jongoo bahari zenye soko dogo kwenye masoko ya jongoo bahari kwenye nchi husika. Bei zake huwa ni chini ya shilingi laki 3 zikiwa kavu kwa kilo moja. Hivyo, biashara ya jongoo bahari duniani huhusisha jongoo zenye thamani kubwa, kupelekea uvunaji holela wa koosafu za jongoo bahari zenye thamani sokoni kutoka kwenye vyanzo vya asili. Nchini China, jongoo bahari huuzwa kwenye maduka yauzayo mazao makavu ya bahari. Wateja mbalimbali hununua jongoo na kuzitumia kwa matumizi ya aidha chakula au kutengeneza madawa ya tiba za asili za kichina au za kifamasia. Hivyo jongoo bahari huchukuliwa kama chakula ghali, hivyo, matajiri na watu wenye vipato vya kati humudu ulaji huo.

Kwanini uvuvi wa jongoo bahari ulipigwa marufuku Tanzania bara.

Sheria ya uvuvi ya awali ya mwaka 1970 iliruhusu uvuvi wa jongoo bahari Tanzania bara. Jongoo bahari waliruhusiwa kuvuliwa na miaka ya 1970 hadi miaka ya 1990 uvuvi wa jongoo bahari ulishamiri maeneo mengi ya Tanzania. Kutokana na ongezeko la uhitaji wa bidhaa hiyo uvunaji wa jongoo bahari ukashamiri kwa kasi bila ya kudhibitiwa. Kukosekana kwa uangalizi madhubuti wa uvuvi wa jongoo bahari katika pwani za Tanzania bara na Zanzibar kukapelekea kupungua kwa kasi kwa idadi ya jongoo bahari kwenye vyanzo vya asili. Kwani jongoo bahari huchukua muda wa mwaka mmoja na zaidi kwa viungo vyake vya uzazi kupevuka na kuweza kuzaliana, kitaalam huitwa ‘Age of sexual maturity’.  Na uzito wa jongoo bahari alivepevuka huwa ni gram 300 na zaidi. Hivyo uvunaji wa jongoo bahari ulipelekea kuvunwa hadi jongoo ambao hawajapevuka yaani chini ya gram 200 na kupelekea kupunguza kasi ya kuzaliana kwa jongoo bahari kwenye vyanzo vya asili.

Hivyo tafiti mbalimbali zilizofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es salaam pamoja na Taasisi ya Tafiti za Uvuvi Tanzania (TAFIRI) miaka ya 2000 zilibaini kupungua kwa kasi kwa koosafu mbalimbali za jongoo bahari kwenye vyanzo vya asili. Tafiti hizi ziliweza kushauri Serikali kipindi hicho kuzuia uvuvi wa jongoo bahari na kupelekea kupitishwa kwa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya 2003 ikitaja jongoo bahari kama miongoni mwa wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka. Sheria hiyo ikatengenezewa Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009 ambazo zimesisitiza katazo la uvuvi wa jongoo bahari kwenye vyanzo vya asili.

Uvuvi wa jongoo bahari bado unatambulika Zanzibar, na kuna jitihada mbalimbali za kudhibiti uvuvi huo na kuufanya endelevu. Makatazo ya uvuvi ya muda kwenye baadhi ya maeneo yenye mazalia ya jongoo bahari, udhibiti wa uzito wa jongoo wanaovuliwa pamoja na usajili wa wafanyabiashara wa jongoo ni miongoni mwa mbinu zinazotumika Zanzibar kudhibiti koosafu za jongoo bahari ili zisipotee. Hivyo ufugaji wa jongoo bahari ulianzia Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 2010 katika hatua za kiutafiti zenye lengo la kufanya uvuvi huu kuwa endelevu.

Ufugaji wa jongoo bahari

Nchi nyingi zimefanikiwa sana katika ufugaji wa jongoo bahari, Nchi kama Japani ambayo ndio ilikuwa kinara wa kuongoza ufugaji wa jongoo bahari miaka ya 1980 kwa ufugaji wa jongoo bahari kwa mfumo wa matenki. Jongoo aina ya spinyo wa kijapani “Apostichopus japonicas” ndio jongoo pekee ambaye hufugika kirahisi kwa mazingira ya matenki. Tafiti nyingi za kiufugaji zimebainisha kuwa ufugaji huu wa aina hii ya jongoo ndio ulifungua njia ya awali ya ufugaji wa jongoo kwa njia ya matenki. Katika ufugaji huu, jongoo bahari hufugwa kwenye mifumo maalum ambayo matenki yenye maji bahari ambayo huingizwa maji kwa njia ya pampu na hewa ya kwenye maji huingizwa kwa njia ya mitambo ya kuingizwa hewa iitwayo kitaalam ‘aerator’. Hivyo ufugaji wa awali wa jongoo ulihusisha ufugaji wa jongoo jamii ya spinyo za kijapani na ufugaji wa jongoo aina ya jongoo maji kwa njia ya matenki.

Ufugaji wa jongoo bahari haswa jongoo maji (Holothuria scabra) uligundulika kuwa unaweza kufanikiwa kirahisi kwa njia ya kuwapandikiza kwenye uzio maalum ambao unaweza kusimikwa baharini. Hivyo nchi za kusini-mashariki mwa bara la Asia kama Malaysia, Indonesia, Vietnam na Ufilipino zilianza kubuni aina mbali mbali za uzio au vizimba mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kupelekea ufugaji wa jongoo maji kukua kwa kasi ukanda huo. Hatimaye jongoo maji wakaweza kuzalishwa kwa wingi kwa njia ya vizimba na kupelekea kuinua uchumi wa bluu katika nchi husika. Barani Africa, ufugaji wa jongoo bahari kwa njia ya vizimba ulianza rasmi mwanzoni mwa miaka ya 2010 nchini Madagascar. Nchini Tanzania, haswa Tanzania bara ufugaji wa jongoo bahari ulianza rasmi mwaka 2019 baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa mwongozo wa kuinua ufugaji wa jongoo bahari, kilimo cha mwani, unenepeshaji wa kaa na kambakoche. Jitihada hizo zikapelekea Kikundi cha kwanza cha ufugaji jongoo bahari Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Tanzania kiiitwacho BMU Kaole. Mpaka sasa vikundi mbalimbali Tanzania bara vimeanza ufugaji wa jongoo bahari.

Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi, FETA Kampasi ya Mikindani pia ilianza majaribio ya ufugaji wa jongoo bahari Mkoani Mtwara mwaka 2021. Majaribio hayo yalileta matokeo chanya na kuchochea kuundwa kwa moduli za mafunzo ambayo zinatokana na elimu, ujuzi na uzoefu wa ufugaji viumbe maji haswa jongoo bahari wa wakufunzi wa Kampasi hiyo. Mkoani Mtwara vikundi kama BMU Namela, Jitegemee group, Mijoba, Bahari Group tayari vimeshaanza ufugaji wa jongoo bahari kwenye hatua za awali baada ya kupokea mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalam wa FETA Kampasi ya Mikindani. Mkoani Lindi, mafunzo mbalimbali na ushauri kuhusu ufugaji wa jongoo bahari tayari umeshaanza kutolewa. Wadau mbalimbali wakiwa kwenye vikundi, makampuni au watu binafsi wameshachangamkia fursa hii kwa ukanda wa kusini.

Kwanini tufuge jongoo bahari kwa njia ya kizimba

Ufugaji wa jongoo bahari kwa njia ya kizimba ni ufugaji rafiki kwa mazingira. Ujenzi wa kizimba huzingatia ikolojia ya bahari ya pwani. Kizimba cha jongoo bahari huruhusu samaki na aina vyingine za viumbe bahari kupita kirahisi bila ya kubugudhi majongoo bahari. Vizimba vya jongoo bahari hutengeneza mazingira ya jongoo bahari wengi kukutana kirahisi katika sehemu moja na kuongeza fursa ya jongoo bahari kuzaliana na kuongeza idadi ya vifaranga vilivyopungua kwenye bahari ya asili.

Idadi ya jongoo wanaopandikizwa huzingatia uwezo wa shamba husika hivyo jongoo wapandikizwao hawana athari za kuchafua mazingira kwa kuongeza kiwango cha taka laini na taka ngumu baharini. Pia, jongoo maji ni wasafisha bahari wazuri ambao kitaalam huitwa ‘Deposit feeders’. Wasafisha bahari hawa hula taka taka za kiorganiki zinazopatikana kwa kutuama kwenye udongo wa baharini, hivyo ufugaji wa jongoo bahari aina ya jongoo maji ni rafiki kwa mazingira kwani inaongeza idadi ya wasafisha bahari na pia huongeza kasi ya kusafisha mazingira ya bahari. Jongoo bahari wanalainisha na kuchanganya udongo wa bahari kama wafanyavyo minyoo aina ya ‘earthworm’ kwa mchakato uitwao kitaalam ‘bioturbation’. Uchanganyaji huu huboresha afya ya udongo wa bahari na kuruhusu viumbe vingine viishivyo kwenye udongo viishi kwenye mazingira bora zaidi.

Namna ya kupata kibali cha kufuga jongoo bahari

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatoa vibali vya ufugaji jongoo bahari vya majaribio kwa miaka 2. Vibali hivi vina lengo la kutambua mfugaji/wafugaji wa jongoo bahari na kuratibu mashamba yao kupitia maafisa uvuvi wa maeneo ya karibu na mashamba yao. Pia, Serikali za mitaa zina majukumu ya kusimamia wafugaji jongoo bahari na kuwatengea maeneo ili kuepusha migogoro itokanayo na matumizi mabaya ya maeneo ya pwani. Mfugaji wa jongoo bahari hatoruhusiwa kujenga kizimba, kupandikiza vifaranga, kuvuna na kuuza jongoo bahari wake bila ya kuwa na kibali husika.

Kibali hiki hupatikana kwa kuandika na kutuma barua ya kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kisha kupitia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika kama ya Jiji, Wilaya, Manispaa au Mji,  kisha kupitishwa kwa Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa halmashauri husika. Pia barua hizi hazina budi kupitia kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji au Mitaa. Barua hiyo iliyokamilika hutumwa Wizarani na kibali hupatikana ndani ya siku 14 bila gharama yoyote. Mfugaji jongoo bahari mwenye kibali atalazimika kukiwasilisha kibali chake kwenye uongozi wa Serikali za Mitaa ili aweze kutambulika rasmi.

Mafunzo ya ufugaji jongoo bahari

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia taasisi yake ya Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) haswa Kampasi ya Mikindani, Mtwara inatoa rasmi mafunzo ya muda mfupi yenye kumjengea uwezo mshiriki kufahamu kinaga ubaga ufugaji wa jongoo bahari, matumizi ya jongoo bahari, uchakataji wa jongoo bahari pamoja na masoko. Mpaka sasa, taasisi hiyo imeweza kutoa elimu ya ufugaji huu kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi na kuwajengea uwezo zaidi ya Washiriki 100 kwenye ufugaji wa jongoo bahari ukanda wa pwani.

Pia, unaweza kupata uzoefu wa kiufugaji kutoka kwa wafugaji wa jongoo bahari wa Kikundi cha BMU Kaole, Bagamoyo Tanzania, ambacho kinasimamiwa na Bw. H. Mahanga. Kikundi hichi tayari kina mafanikio makubwa katika ufugaji huu wa jongoo bahari kwa zaidi ya miaka 3. Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada mbalimbali za kuongeza wataalam wenye ujuzi wa ufugaji jongoo bahari na kuanzisha maabara za kutotoleshea vifaranga vya jongoo Mkoani Tanga, Dar es salaam na Mtwara.

Namna ya kuanzisha shamba la jongoo bahari

Eneo la kufuga jongoo bahari lazima liwe lina sifa zote ambazo zitamwezesha jongoo bahari haswa jongoo maji “Holothuria scabra” au kwa kingereza ‘sandfish’ kuishi na kunawiri kipindi chote cha msimu. Uchaguzi wa eneo la bahari huzingatia misimu ya kupwa na kujaa kwa bahari. Haswa misimu mikuu ya bamvua ‘spring tide’ na maji mafu ‘neap tide’. Umakini pia unahitajika kubaini aina ya udongo wa eneo la bahari ambalo kizimba kitajengwa na mashamba ya jongoo bahari kuwekwa. Kwani aina mbaya ya udongo wa bahari huweza kumsababishia majeraha ya kuchunika ngozi jongoo maji.

Eneo la pwani lenye sifa bora za kufuga jongoo likishapatikana, ni muhimu uongozi wa serikali za mtaa haswa serikali za vijiji kupewa taarifa juu ya uanzishwaji wa shamba la jongoo bahari. Shamba la jongoo bahari huundwa na vizimba vya kufuga jongoo bahari ambavyo huundwa kwa nyavu za plastiki au migono ya kutumia miti maalum isiyooza baharini. Kisha wavu huo husimikwa katika namna itakayozuia jongoo kutoroka kutoka kwenye kizimba. Kizimba kimoja chenye uwezo wa kuzalisha kilo 60 kavu za jongoo bahari hakina budi kiwe cha eneo la robo ekari yaani mita mraba 900. Kisha idadi maalum ya jongoo kwa kizimba husika hupandikizwa mwanzo wa msimu.

Namna ya kusimamia shamba la jongoo bahari

Mbinu mbalimbali hutumika katika usimamizi wa shamba la ufugaji jongoo. Kubaini uwezo wa shamba lako ni muhimu kwani itakujulisha idadi ya vifaranga vya kupandikizwa na muda sahihi kwa kuvuna zao lililokomaa kizimbani. Muda wa jongoo bahari kuvunwa hutofautiana kati ya shamba moja hadi jingine kwani jongoo bahari kufika uzito wa kibiashara wa gram 300 huchukua muda wa miezi 6 hadi 9 akiwa kwenye kizimba/shamba. Mashamba mengi ya jongoo bahari ya vizimba huvuna jongoo wenye kuanzia gram 300 hadi gram 650. Uratibu na ukaguzi wa shamba la jongoo bahari ni muhimu ili kudhibiti idadi ya jongoo bahari. Idadi ya jongoo bahari ikidhibitiwa vizuri huongeza kasi ya faida kwenye mavuno ya mwisho wa msimu.

Ukarabati wa kizimba cha kufugia jongoo bahari na kudhibiti maadui wa jongoo bahari ni jambo muhimu katika kudhibiti idadi ya jongoo bahari na kuongeza kasi ya ukuaji wa jongoo bahari kwa kuruhusu ongezeko la chakula cha asili cha jongoo bahari. Kumbuka ufugaji wa jongoo bahari kwa njia ya kizimba una faida kubwa tofauti na ufugaji wa samaki kwani jongoo akishapandikizwa kwenye kizimba halishwi chakula cha ziada yaani ‘supplementary feeds’ hivyo gharama ya manunuzi ya chakula huingia moja kwa moja kwenye faida ghafi ya mfugaji jongoo bahari kwenye msimu.

Kudhibiti upotevu wa mazao ya jongoo bahari

Udhibiti wa upotevu wa mazao au kitaalam “Post harvest loss control” ni mbinu zote zinazotumika kuzuia chakula kisioze au kuharibika haraka kabla hakijamfikia mteja. Tofauti na samaki, jongoo bahari mara nyingi hauzwi kwenye hali ya ubichi bali anauzwa akiwa kwenye hali ya ukavu ambayo kitaalam ambayo inaitwa ‘Beche de mer’. Hali hiyo humuwezesha jongoo aliyevunwa kuhifadhika kwa muda mrefu zaidi akiwa sokoni. Mbinu mbalimbali hutumika kwa ajili ya kumuandaa jongoo bahari aweze kuhifadhika kwa urahisi. Jongoo akishavuliwa hutolewa utumbo kwa umakini mkubwa ili kudumisha umbile la jongoo mwisho wa uchakataji. Jongoo huyo huifadhiwa kwenye chumvi na kuchemshwa kwa maji bahari na kukaushwa juani. Umakini unahitajika katika kujua unamu ‘texture’ wa jongoo wakati wa kumpika na kumuanika ili kupata zao bora litakalofaa sokoni.

Mbinu hizi za upikaji wa jongoo bahari zinafahamika na baadhi ya watu wa ukanda wa pwani waliojihusisha na biashara hiyo hapo awali kabla ya kupigwa marufuku. Uangalifu mkubwa unahitajika wakati wa zoezi hili la kumuandaa kwani uandaaji mbaya wa jongoo unaweza kumfanya jongoo atoke akiwa kwenye umbile lisilovutia kwenye soko, kwani umbile lenye mvuto mkubwa sokoni ni umbile la soseji. Kisha jongoo huhifadhiwa kwenye viroba au maboksi na huweza kusafirishwa kwenda kwenye masoko ya Uchina, Thailand, Korea, Japani na Marekani.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here