Home MAKALA MAFUNZO ZIADA KUTOKA KIFO CHA MZEE MWINYI

MAFUNZO ZIADA KUTOKA KIFO CHA MZEE MWINYI

Google search engine

*Alitekeleza amana ya uongozi zama zake

Alhaj Ali Hassan Mwinyi

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MAREHEMU Alhaj Ali Hassan Mwinyi ni Sheikh, kifo chake si msiba tu bali pia ni jukwaa la mawaidha, nasaha na mahubiri.

Kama alivyonena Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwamba ameunguliwa na maktaba, kwetu sote ni msiba unaotuachia tafakuri  kwamba, hata ingalikuwa wanaadamu wamejaaliwa umri mrefu zaidi ya ule alioishi Adamu, Nuhu na wengineo waliotangulia katika kizazi chao bado maisha ya ulimwengu huu yasingelikuwa na maana yoyote kama pasingelikuwa na uumbaji na lengo la kuumba.

Wala maisha hayo yasingeliwahakikishia wanaadamu na viumbe vingine furaha na starehe ya kudumu.

Miaka 99 kasoro aliyoishi Mzee Mwinyi na zaidi ya huo kidogo,  ndio umri mrefu ambao Mwanaadamu wa zama hizi aliyejaaliwa kuufikia husemwa ‘alhamdulillah’ marehemu kaishi.

Katika umri huo, Wanasaikolojia wanaeleza  ni kipindi cha utotoni tu cha mwanaadamu huyu kikongwe, yaani tangu umri wa 0 hadi miaka 14 ambao pengine aliweza kuishi kwa furaha ya hapa na pale ingawa hata hivyo wanakiri  ni wachache mno wanaobahatika kuishi mazingira ya furaha.

Wanasaikolojia wanaeleza lipo kundi la wachache zaidi kuanzia miaka 15 hadi 30 ambao wakati fulani hupata fursa ya kuishi kwa “furaha”.

Hata hivyo maana ya furaha kwa mnasaba wa maisha haya ni  kuridhika, kutokuwa na hofu na kujihakikishia kupata mahitaji ya msingi ya kibinaadamu.

Mitazamo mingine ya furaha ni ya kiuchumi zaidi kuliko kinafsi na kisaikolojia ambapo wachache wenye furaha ni wale wanaoishi kwenye mazingira mazuri ya kiuchumi ambao fursa yao ya kuwa na “pesa” huwawezesha kula, kunywa, kulala pazuri, kustarehe pasi na misongo, kutatizwa, kutingwa au kukwazwa na majukumu mbali mbali ya kifamilia au kijamii.

Wanasaikolojia wanasema kwa kadiri maisha yalivyo, furaha itokanayo na uchumi mzuri hukatizwa na mitihani ya maradhi, uzee chambilecho Mzee Mwinyi akizungumza katika msiba wa Hayati John Magufuli kule Chato kwanza aliuliza hapa tuko wapi, kisha alisema, ‘nimekuwa mzee mno’.

Aidha kuna ajali mbali mbali,  kuuguliwa, kufa kwa muhusika au kufiwa na ndugu au jamaa.

Hali hizi kisaikolojia inaelezwa hubadilisha furaha kuwa huzuni pengine ghafla.

Saikolojia ya huzuni mara nyingi husababishwa na  taarifa au matukio fulani yasiyopendeza kwa mtazamo au matakwa ya muhusika.

Uzoefu unaonesha wakati fulani watu wa familia fulani wanaweza kuwa kwenye furaha ghafla wakajikuta wakihanikizwa na majonzi au huzuni kutokana na pengine msiba uliotuka katikati ya shangwe na hoi hoi iliyokuwa ikitafsiri furaha yao.

Miaka kabla ya 40, ni umri wa utu uzima wa katikati ambao pengine Mwanadamu huyu au yule aliweza kupata fursa ya kuishi kwenye hali na mazingira yaliyotafsiri istilahi ya “furaha”.

Hata hivyo, kipindi chote kilichoendelea kufikia miaka yake 100, kwa waliobahatika kufika umri huo, bila shaka kilikuwa cha misongo, huzuni, adha, taabu, maradhi, wajibu na kuwajibika kwa ajili yake mwenyewe, Kwa wengine, kifamilia au kijamii.

Hatimaye Mwanaadamu huyo humalizia  umri ulioitwa “mrefu” katika hali dhalili ya uzee ulioandmana na magonjwa ya kizee na kisaikoljia.

Umri huo dhalili humlazimisha Mwanaadamu  kuwa duni na tegemezi wa kuhitaji msaada kwa kila jambo.

Kwa ufupi Mwanaadamu huyu, katika uhai wake wote, ameishi muda mfupi sana wa furaha na muda “mrefu” wa adha, taabu na huzuni kama Qur’an inavyobainisha:

“Tumemuumba Mwanaadamu katika taabu”(90:4)

Kwa upande mwingine, kanuni za sayansi halisi za tangu na tangu pamoja na hatima ya vitu vyote sanjari na maarifa yahusianayo na maumbile, yanaonesha kuwa, upatanifu kati ya Mwanadamu na maumbile asilia umevurugwa na kusababisha nakama (dhwanka) kubwa zaidi katika maisha haya ya dunia.

Kwa hakika hakuna jamii inayoweza kuwa na amani au furaha muda wa kuwa tabia za wanajamii wake zimemili zaidi kwenye utovu wa maadili, uovu, ufisadi, shari na dhambi kama ilivyo sehemu mbali mbali duniani hivi sasa.

Kwa ufahamu huu, akili ya kawaida ingepaswa kuleta msukumo wa kuhoji kwa nini basi wawepo wachache sana wanaotanabahi.

Kwa nini wengi wasiwe wenye kumili kutenda mema, wema, uadilifu, huruma, uungwana, kuguswa na kutaabishwa na matatizo ya wengine, kama inavyojitokeza katika maisha ya marehemu Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Watu watafute maisha mengine ya furaha zaidi Kwa kutenda mema historia ije kuwakumbuka kama anavyokumbukwa Ali Hassan Mwinyi.

Watu watafute maisha yajayo yasiyo na wajibu, kuwajibika wala kuwajibishwa, maisha yasiyo na huzuni, adha, taabu, misongo wala matatizo mengineyo.

Kwa hakika kila Mwanaadamu mwenye akili timamu angetamani maisha hayo, kila mmoja angetamani uhai wa milele akiwa katika raha na starehe.

Lakini vipi na wapi maisha hayo yatapatikana?

Wenye tafakuri watanabahi kuwa kaburi si nyumba ya milele wala si kila Mwanaadamu atapumzika kwa amani baada ya kifo.

Wenye tafakuri sahihi wadhamirie kuishi maisha ya furaha ya kweli ya mwili na roho huko Akhera.

Wenye Akili na tafakuri inayotokana na mawaidha ya vifo kama hikincha Mzee Mwinyi na wengineo wanawajibu wa kuondoa matatizo yaliyosababishwa na uharibifu wa ulinganifu kati ya mwanaadamu na maumbile hapa duniani.

Wana wajibu wa kutekeleza ipasavyo dhamana walizokabidhiwa kifamilia na kijamii.

Wataweza kufanya hivyo iwapo wataweka au kuandaa mazingira elekezi na yenye kushawishi njia mbadala mahala pa uasi na ukiukaji kanuni halisi za Muumba.

Wataweza kufanya hivyo iwapo watavaa nyoyo na kuiga mazuri ya wema waliowatangulia katika jami zaoi, marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa mmoja wa wema hao.

Buriani Mzee Mwinyi, Buriani Mzee Rukhsa.   Buriani Rais mstaafu wa Awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uliwatoa  watanzania kwenye pekupeku, katambuga, makubazi, sandarusi, “karumanzila” na “kibena mjanja”, ukawavika raba “mtoni”, mokasini, sendles anuai’ na nguo za thamani.

Uliondoa muhongo uliooza, mchele mdundiko na kitumbo, ukarejesha supa na kuketa pishori juu, bidhaa nyingine tele madukani.

Uliwatoa Watanzania kwenye njaa Kali, ukawalisha milo kadhaa kutoka mlo mmoja kwa siku,  chai ya sukari guru, sabuni bidhaa adimu kwa foleni,, ukajaza bidhaa tele madukani.

Una malipo yako makubwa Kwa wema huo. Buriani Ali Hassan Mwinyi

Hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu  na kwake yeye tutarejea

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here