Na Joseph Mahumi WFM, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, amewahakikishia wafanyabiashara na makampuni binafsi kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuwawezesha kuendelea kuwekeza na kukuza uchumi wa nchi.
Bw. Lawrence Mafuru ametoa ahadi hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Takashi Araki.
Mafuru alisema Sekta Binafsi ina imani na Serikali hali ambayo inawawezesha wawekezaji kuwa na uhakika na mipango yao.
“Kampuni ya Sigara nchini wamefurahishwa na Sera za usimamizi wa uchumi ambazo zimeendelea kuboreka na kuwawezesha kufanyabiashara yenye tija”, alisema Mafuru.
Alisema pia kuwa Kampuni hiyo umeelezea kufurahishwa kwao na mazingira ya siasa yalivyo, ambayo yanaruhusu amani na utulivu huku wakiiomba Serikali kuangalia vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha ufanyajibiashara nchini kwa ufanisi zaidi.
Alisema wameshauri Serikali iangalie suala la kodi kwa kuwa na kodi ambazo zinatabirika na zisizobadilikabadilika kila wakati pamoja na kuangalia mazingira mengine ya ufanyaji biashara.
Nae Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Takashi Araki alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi wa nchini huku akisisitiza kuhusu kujenga uaminifu kati ya Serikali, Sekta Binafsi na wananchi.
Alisema ni jambo la msingi kuwa na uchumi unaokua na kuhusisha maendeleo ya watu, hivyo anatamani Tanzania iwe na uchumi thabiti.