Na MWANDISHI WETU
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (TIRA), pamoja na Benki ya CRDB kwa kutekeleza mchakato wa uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima (Trust Account).
Mafuru ametoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya utekelezaji wa akaunti hiyo kwa Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Wakuu wa Fedha wa makampuni ya bima nchini yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.
Mafuru amesema uanzishwaji wa Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima uendana na matakwa ya kisheria na udhibiti yaliyowekwa na TIRA.
Akielezea changamoto za hapo awali, Mafuru amesema utaratibu uliokuwa ukitumika mwanzoni katika usimamizi wa dhamana ya bima haukuwa mzuri jambo ambalo lilipelekea TIRA kushindwa kusimamia vizuri amana hizo pindi ziliporejeshwa kwa makampuni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) baada ya kuiva.
Amesema kuwa kampuni nyingi za bima zilikuwa zikitumia fedha za amana ya Akiba katika matumizi mengine, pasipo kupata idhini ya TIRA hivyo kupelekea kuingia katika changamoto ya ukwasi, na wakati mwengine kushindwa kulipa fidia kwa wateja kutokana na fedha kuwekezwa katika miradi mingine.
Mafuru alibainisha kuwa uamuzi wa kufungua Akaunti ya Dhamana ya Bima katika benki za biashara ni mwarobaini wa changamoto hiyo, kwani sasa TIRA itaweza kusimamia moja kwa moja fedha hizo za amana za akiba, jambo ambalo si tu litaimarisha usimamizi, bali pia kuboresha maendeleo ya sekta ya fedha.
“Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuwa benki ya kwanza kuungana na TIRA katika uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba. Lakini nimevutiwa na namna ambavyo mmeona kuna umuhimu wa kuandaa mafunzo haya ambayo yanalenga kuwajengea uelewa makampuni ya bima juu ya uendeshaji wa akaunti hiyo,” amesema Mafuru.
Aidha, Mafuru alimtaka Kamishina wa TIRA kuhakikisha kampuni zote za bima zinafuata sheria kwa kuweka dhamana ya amana. Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuchochea mafanikio ya sekta ndogo ya bima kama ilivyoanishwa katika Mpango wa Taifa wa miaka 10 wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini ‘Financial Sector Development Master Plan’.
Akizungumza katika warsha hiyo, Kamishina wa Mamlaka ya Bima, Dk. Baghayo Saqware amesema chimbuko la Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 inayozitaka Kampuni za Bima kuweka Amana za Usalama angalau asilimia 50 ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima.
Dk. Saqware amesema mwaka jana Mamlaka kwa kushirikiana Chama cha Watoa Huduma za Bima (ATI), walikubaliana kuandaa Mwongozo wa Uwekazaji wa Usimamizi wa Ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.
“Mfumo unaokwenda kutumika katika akaunti hii mbali na kuboresha usimamizi, lakini pia ni rafiki na unaleta uwazi zaidi kwa wadau kwa maana ya kampuni za bima. Makampuni yataweza kupata taarifa ya dhamana kwa wakati, na kufanya uwekezaji kulingana na makubaliano na Mamlaka,” aliongezea Dkt. Saqware.
Akitoa taarifa za utendaji wa sekta ya bima, Dk. Saqware alimjulisha Naibu Katibu Mkuu kuwa sekta hiyo imeendelea kukua kulinganisha na miaka iliyopita. Amesema mwaka jana mauzo ya bima yaliongezeka kwa asilimia 25 kufikia Shilingi Trilioni 1.146 kulinganisha na mauzo ya 2021. Aidha, alibainisha kuwa malengo ya mwaka huu ni kufikia Shilingi Trilioni 1.5.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, ameishukuru TIRA kwa kuipa fursa ya kushiriki katika uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima. Nsekela alipongeza uamuzi wa uanzishwaji wa akaunti hiyo na kusisitiza kuwa inachukua jukumu muhimu katika kukuza uwazi zaidi na uwajibikaji katika sekta ya bima, na kuwa itakwenda kusaidia pia kujenga imani kwa wadau wa sekta hiyo.
Nsekela Akaunti ya Dhamana ya Bima iliyofunguliwa Benki ya CRDB imezingatia kwa asilimia mia moja mapendekezo ya TIRA na wadau wa sekta ya bima, huku akibainisha kuwa akaunti hiyo imeunganishwa na mifumo ya kidijitali itakayosaidia katika usimamizi na utoaji wa taarifa kwa Mamlaka na kampuni za bima.
“Kwa kuzingatia kuwa fedha hizi pia zimekuwa zikitumika kwa uwekezaji wa makampuni, Benki yetu imejipanga kikamilifu katika kutoa ushauri na usaidizi wa uwekezaji kupitia Idara yetu ya Hazina na Masoko ya Mitaji,” amesema Nsekela.
Nsekela alimuhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa Benki ya CRDB itaendelea kushirikiana na TIRA na wadau wa sekta ya bima kusaidia Kuboresha sekta hiyo. Nsekela alisema Benki hiyo imekuwa kinara katika utoaji wa huduma za bima kupitia mfumo wa BancAssuarance, huku akibainisha kuwa imekuwa ikitoa huduma hizo katika matawi yake, CRDB Wakala, na kidijitali kupitia SimBanking.