Home KITAIFA Grumeti Fund bega kwa bega, wasichana Serengeti wahimizwa kujilinda kufikia ndoto zao

Grumeti Fund bega kwa bega, wasichana Serengeti wahimizwa kujilinda kufikia ndoto zao

Google search engine
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Neema Msuya akizungumza na wasichana waliohudhuria katika kongamano la wasichana lilofanyika hivi karibuni katika Shule ya sekondari Issenye

NA MWANDISHI WETU

SERENGETI, MARA.

KAMPUNI ya Grumeti Fund kupitia Idara yake ya Maendeleo ya Jamii imeendelea kutoa semina kwa vijana wakiume na wakike Wilayani Serengeti na Bunda ambapo mpaka sasa imefikia mabinti 9,308 na vijana wa kiume 1,018 kuanzia 2017- 2022.

Katika semina hizo mabinti 9,308 kutoka Sekondari 19 za Wilaya ya Bunda na Serengeti, walipewa taulo za kike za kutumia kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita.

Katika kongamano hilo lilofanyika Mwanzoni Mwa wiki Hii, vijana wa kike wameaswa kujituma na kuepuka vishawishi ili kutimiza ndoto zao na kuwa msaada katika Taifa huku ikitoa taulo za kike 761 zinazoweza kufuliwa na kudumu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu kwa wasichana wote 761 waliohudhuria semina hiyo.

Akizungumza na wasichana hao katika kongamano hilo, Mgeni rasmi Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Neema Msuya ameipongeza kampuni ya Grumeti Fund kwa kuona umuhimu wa kufanya makongamo hayo na kuwataka wasichana hao kutekeleza yote waliyojifunza ili kutimiza ndoto zao.

“Nawashukuru sana Grumeti Fund, tunatumaini kwa juhudi za wadau hawa  hakutuwa na utoro mashuleni, mimba za utotoni, ndoa za mapema na ukeketaji.

“Nyinyi mpo kwenye safari ya maisha, safari bado ni ndefu mkawe na ujasiri, uthubutu, mjiamini mkawe watu bora” amesema Neema

Aidha, ametoa wito kwa mashirika, kampuni na taasisi nyingine kuiga mfano wa Grumeti Fund katika kuendesha semina na makongamano ya kufundisha vijana wa kiume na wakike katika maeneo mbalimbali ili kuwasaidia katika maisha yao.

“Grumeti Fund, naomba muendelee kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo katika Wilaya yetu ya Serengeti na Taifa kwa ujumla” amesema Neema.

Kongamani hilo  limehusisha wasichana kutoka shule za Sekondari Issenye, Nagusi,na Rigicha za wilayani Serengeti.

Aidha, amewataka wasichana hao kujituma kielimu  na kiujasiriamali ili kutimiza ndoto zao  kwa sababu ya uwepo wa mazingira rafiki na  amewasihi kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika maisha yao na kuepuka makundi hatarishi na tamaa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii  Grumeti Fund, Frida Mollel amewakumbusha wasichana hao kuwa wana haki ya kusema hapana kwa mila na desturi potofu ambazo zinawakandamiza na kuwapotezea fursa mbalimbali za kimaisha ikiwemo masomo.

“Mwanamke au binti unanafasi kubwa sana katika jamii kufanya mabadiliko ya kiuchumi, kielimu, na kisayansi,’’ alisema

Frida amewasisitiza mabinti kuwa wanaweza kufanya chochote na kuwa mtu yeyote na  kutimiza ndoto walizonazo, ikiwa watasimama kidete kusimamia maisha yao na kuacha kukumbatia vitu vinavyokwamisha ndoto zao ikiwemo mimba zisizotarajiwa, makundi rika, utoro, ndoa za utotoni na kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii.

Pia ametoa wito kwa wazazi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia katika  ujenzi wa miundombinu mbalimbali yakiwemo madarasa na mabweni ili kuboresha elimu zaidi na kufanya watoto kuwa salama.

Grumeti Fund hualika wadau mbalimbali kutoka katika asasi za kijamii ili kuzungumza na mabinti katika maeneo mbalimbali ya maisha yao wakati wa kongamano.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa Chuo cha  Sayansi za afya Kisare, Mwalimu Restuda Murutta, amewataka wasichana hao kuepuka ndoa za utotoni, mimba zisizotarajiwa na kudumisha usafi haswa kipindi cha hedhi.

“Tujifunze kujitunza ili kuepuka mimba za utotoni ili kuepuka madhara yatokanayo na kubeba mimba mapema, lakini pia tukumbuke kuweka mazingira yetu ya choo safi ili tusipate magonjwa.’’alisema Mwl Restuda

Naye Mkurugenzi wa kituo cha nyumba Salama, Hope for Girls and women in Tanzania, Rhobi Samweli ametoa wito kwa wasichana  hao kupinga ukeketaji na kuwa chachu ya mabadiliko  kwa kuielimisha jamiii juu ya madhara ya ukeketaji na kutoa taarifa ya vitendo vya ukeketaji,

Kupitia Kongamano hilo wasichana hao walipata wasaa wakuwasilisha changamoto wanazopitia ikiwa ni pamoja na kutoa maoni yao ya namna changamoto hizo zinavyoweza kutatuliwa.

Changamoto hizo ni pamoja na ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia  kama ukeketaji, kunyimwa haki ya elimu, vishawishi, mila na desturi potofu na kubaguliwa.

Grumeti Fund imekuwa ikitoa ufadhili wa kimasomo kwa vijana, elimu ya ujasiriamali na mazingira kwa jamii pamoja na uhifadhi wa wananyama pori.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here