Home KIMATAIFA Ethiopia yaondoa mashtaka dhidi ya viongozi wa Tigray

Ethiopia yaondoa mashtaka dhidi ya viongozi wa Tigray

Google search engine

Serikali ya Ethiopia imetangaza kuwafutia mashtaka ya jinai viongozi wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF), kulingana na makubaliano ya amani ya jimbo hilo la kaskazini mwa nchi hiyo.

Wizara ya sheria ya Ethiopia ilisema Alhamisi kwamba kulingana na makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwezi Novemba nchini Afrika Kusini, mashtaka ya jinai yaliyofunguliwa dhidi ya viongozi wa jimbo la Tigray yameondolewa kama sehemu ya makubaliano hayo.

Tangazo hilo ndilo la hivi karibuni la hatua za kuimarisha imani chini ya mkataba huo wa amani.

Wiki iliyopita, serikali ya Ethiopia ilisema imemteua afisa wa ngazi ya juu wa TPLF kuongoza utawala wa mpito wa jimbo la kaskazini Tigray,

Uteuzi huo ulifanyika siku moja baada ya bunge kukiondoa chama cha TPLF katika orodha rasmi ya mashirika ya kigaidi.

Getachew Reda ameteuliwa kuwa rais wa utawala wa mpito wa Tigray

Katika juhudi za kurejesha amani kote Ethiopia, hivi majuzi Waziri Mkuu, Abiy Ahmed alisema serikali yake ina nia ya kweli vilevile kutatua kwa amani mgogoro kati yake na kundi la waasi la Jeshi la Ukombozi la Oromo (OROMIA). Alisema tayari kumeundwa kamati iliyopewa jukumu la kuongoza mchakato huo akitumai kuwa raia wa Ethiopia wataiunga mkono hatua hiyo.

Mgogoro wa Tigray ulianza Novemba mwaka 2020, wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alipopeleka vikosi vyake kupindua utawala wa chama cha TPLF katika jimbo hilo, akiwashutumu wapiganaji wake kuzishambulia kambi za jeshi la serikali ya shirikisho.

Marekani na Ethiopia wajadili uwajibikaji huko Tigray

Mnamo Novemba mwaka 2020, shirika rasmi la habari linalomilikiwa na serikali ya Ethiopia, liliripoti kwamba waranti umetolewa kukamatwa kwa viongozi 64 wa TPLF na wanajeshi 32 wa ngazi ya juu, pamoja na maafisa wa polisi jimboni humo kwa tuhuma za uhaini.

Katika kipindi cha vita, wakati mmoja wapiganaji wa Tigray walisogea karibu mji mkuu Addis Ababa, lakini walishambuliwa na vikosi vya Abiy na kulazimika kurudi nyuma

Miongoni mwa waliotajwa kushtakiwa ni Getachew Reda, ambaye wiki iliyopita aliteuliwa kuwa ‘rais wa utawala wa mpito wa jimbo hilo’ chini ya makubaliano ya amani.

Ni vigumu kubaini idadi kamili ya vifo vilivyotokana na machafuko hayo ya miaka miwili, lakini Marekani inakadiria kuwa takriban watu 500,000 waliuawa.

Idadi hiyo ni juu kuliko wale ambao wameuawa kwenye mgogoro wa Ukraine, tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari, 2022.

Chanzo: AFPE

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here