Home KITAIFA CCM yawaweka matumbo joto waliotajwa ripoti ya CAG, Takukuru yataka hatua za...

CCM yawaweka matumbo joto waliotajwa ripoti ya CAG, Takukuru yataka hatua za waliohusika

Google search engine

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imeielekeza Serikali kuchukua hatua thabiti kwa wahusika wote waliobainika kuhusika katika ukiukaji wa sheria na kusababisha ubadhirifu wa mali na rasilimali za nchi kwenye ripoti ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Hayo yamesemwa leo Aprili 1,2023 jijini Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa -Itikadi na Uenezi Sophia Mjema mara baada ya Kamati kukutana katika kikao chake cha kawaida chini ya Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mjema amesema Kamati Kuu imetoa maelekezo kwa Serikali kuwafuatilia watu wote wanaotumia dhamana za uongozi vibaya na kushindwa kuweka maslahi ya nchi na uzalendo mbele katika nafasi walizoaminiwa kutumikia watu, badala yake wanaweka maslahi binafsi.

Aidha amesema Kamati Kuu imepokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taarifa ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mwaka wa fedha 2021/22, zilizowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.

Mjema amesema katika taarifa zote mbili ilibainika kuwepo kwa maeneo ambayo taarifa zote mbili zimeonesha Serikali imeboresha na kuendelea kuimarisha kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi, ikiwemo udhibiti na umakini katika matumizi ya fedha za umma, ambapo katika taasisi zilizokaguliwa, asilimia 96 zimepata hati safi.

“Katika mjadala huo wa kina, Kamati imesikitishwa na kuwepo baadhi ya maeneo mengine ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuondoa mapungufu/udhaifu uliobainishwa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya malipo na ukusanyaji wa mapato kutokusomana, kuwepo kwa baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu”. Amesema

Katika hatua nyingine Kamati Kuu  imeipongeza Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa kufanya kazi zao kwa weledi na kuendelea kutimiza wajibu wao kwa taifa.

Hiyo inatokana na kuonesha maeneo ambayo Serikali imeyaboresha na kubainisha madhaifu yanayohitaji kufanyiwa kazi, kwa lengo la kulinda mali, rasilimali kwa maslahi ya taifa.

Akizungumza kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani  Kamala Harris ,Mjema amesema Kamati Kuu, imeipongeza Serikali kwa kuratibu na kufanikisha vema ziara hiyo ya Makamu wa Rais wa Marekani ambaye alikuwepo nchini kwa siku tatu.

Amesema ziara hiyo imeongeza uimara wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani na kufungua milango zaidi ya uhusiano wenye faida kwa maendeleo na ustawi kwa pande zote mbili, hususan katika maeneo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kukabiliana na magonjwa, uchumi, uwekezaji na ajira.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here