Home KITAIFA Wahariri fanyeni kazi zenu bila woga- Rais Samia

Wahariri fanyeni kazi zenu bila woga- Rais Samia

Google search engine

Waziri wa habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari, Nape Nnauye akimkabithi Kaimu Meneja tawi la NMB Wami Paul Nyoni (kulia) Cheti cha shukrani wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 12 wa mwaka wa kitaaluma wa wahariri wenye kauli mbiu ya “Sheria ya habari na maendeleo ya vyombo vya habari” unaofanyika mkoani Morogoro. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deudatus Balile (kushoto) na Makamu Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri, Bakari Machumu (wapili kulia). Benki ya NMB ilishiriki kama mdhamini kwenye mkutano huo unaoendelea hoteli ya Morena, Morogoro

*Akoshwa na maendeleo tasnia ya habari nchini

Na Bakari Kimwanga, Morogoro

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka wanahabari nchini kufanya kazi zao bila woga, upendeleo, uonevu kwa kutanguliza weledi, uzalendo, Katiba ya nchi.

Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa kudumisha amani, utilivu na maendeleo ya nchi.

Rais Dk. Samia aliyasema hayo kupitia salamu zake kwa Wahariri wa vyombo vya habari wanaoshiriki mkutano wa kitaaluma wa 12 unaoendelea mkoani Morogoro.

Mkutano huo ambao unajadili maendeleo ya kitaaluma na kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya habari, umeandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Salamu za Rais Dk. Samia ziliwasilishwa na mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, wakati akiufungua mkutano huo.

Nnauye alisema, pamoja na changamoto zilizopo katika sekta ya habari, serikali ya awamu ya sita inaendelea kuzifanyia kazi, Rais Dk. Samia anafurahishwa na maendeleo makubwa yanayoendelea kupatikana.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuchochea maendeleo ya nchi, jamii na kuimarisha utawala bora,” alisema.

Alisema Rais Dk. Samia ni muumini wa haki ya kutoa maoni, kujieleza hivyo haoni sababu ya kubinya uhuru wa vyombo vya habari.

Aliongeza kuwa, serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia inafurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya TEF na taasisi nyingine za kihabari ili kulijenga Taifa katika umoja, uzalendo, upendo na mshikamano.

“Serikali itaendelea kuwa karibu na vyombo vya habari, kutatua changamoto zao, kuhakikisha jamii inatambua, kuiheshimu tasnia ya habari,” alisema.

Nnauye alisikitishwa na kitendo cha baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari kutolipa mishahara ya Wahariri na waandishi waliopo katika vyombo vyao na madeni jambo linalowafanya wawe ombaomba.

Aliwataka wanahabari kufanya kazi kwa weledi, uzalendo wakitanguliza maslahi ya nchi ili kuipa nafasi serikali itekeleze wajibu wake kwa wananchi.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here