Home KITAIFA BOHARI YA DAWA YAJA NA MAGEUZI MAKUBWA NCHINI

BOHARI YA DAWA YAJA NA MAGEUZI MAKUBWA NCHINI

Google search engine

MAKUSANYO YA FEDHA KWENYE VITUO VYA HUDUMA ZA AFYA KWENDA MSD YAFIKIA SHILINGI BILIONI 118.9 MWAKA 2022/23

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai, akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo Julai 3, 2024, Jijini Dodoma

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

BOHARI ya Dawa (MSD), imetangaza mageuzi makubwa ikiwamo kuimarisha utendaji wake na uwekezaji wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhiwa dawa na vifaa tiba.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali leo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema kuwa Bohari ya Dawa inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 8,224 kutoka vituo 7,662 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la vituo 562 nchini kupitia Kanda zake 10 zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.

Pamoja na hali hiyo amesema kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake.

Ameyataja mafanikio hayo kuwa ni kuongezeka kwa utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya hasa kwa Dawa,Vifaa,Vifaa Tiba na Vitendanishi.

Amesema Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya yanatimizwa kwa mujibu wa maombi yao. Kutokana na kuimarika kwa utendaji, utimizaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma za afya umeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2022/23 hadi kufikia asilimia 84 mwaka 2023/24 na hivyo bidhaa nyingi kuweza kupatikana kupitia MSD.

“Bohari ya Dawa (MSD) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya iliyoanzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Sheria ya Bohari ya Dawa Na.13 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2021 ikiwa na majukumu manne ambayo ni  Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za umma na binafsi zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

“Sambamba na hilo, MSD imeendelea kufanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za Kibingwa na Ubingwa Bobezi nchini kama mashine za kusafisha damu (Dialysis Machine), MRI, CT- Scan, Ultrasound, Digital X-Ray pamoja na vitendanishi vyake. Uwepo wa vifaa hivi unawezesha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi,” amesema Tukai

Kutokana na hali hiyo Mkurugezi huyo wa MSD amesema kuwa mafanikio mengine ni kupatikana kwa mtaji wa uendeshaji kiasi cha Shilingi bilioni 100 kwa mwaka wa Fedha 2023/24, Serikali imetoa kiasi cha Shilingi bilioni 100 kama mtaji wa kuwezesha MSD kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi.

Amesema fedha hizo zimesaidia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati na kuweza kutengeneza mikakati itakayofanya taasisi iweze kununua kwa tija na kuimarisha mahusiano na wazabuni mbalimbali.

“Kuimarika kwa makusanyo ya fedha kutoka vituo vya kutolea huduma za afya ikiwamo maboresho yanayoendelea yamewezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na imani na utendaji wa MSD ambapo makusanyo ya fedha yatokayo kwenye vyanzo mbalimbali vya vituo vya kutolea huduma za afya na kuletwa MSD yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 40.3 mwaka 2022/23 na kufikia kiasi cha Shilingi bilioni 118.9 kwa mwaka 2023/24.

“Kuongezeka kwa Mapato ya MSD kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali, Mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 359.6. kwa mwaka 2022/23, hadi kufikia zaidi ya kiasi cha Shilingi bilioni 510.07 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 150.43 ambayo ni sawa na asilimia 42,” amesema

SERA YA VIWANDA

Amesema katika kutekeleza sera ya uanzishwaji wa viwanda, Bohari ya Dawa imechukua hatua adhaa ikiwamo uanzishaji wa Kampuni Tanzu

Tukai amesema katika kuongeza ufanisi wa usimamizi na uendeshaji wa shughuli za uzalishaji, MSD imeanzisha Kampuni Tanzu inayoitwa “MSD Medipharm Manufacturing Company Limited”.

“Juni 2024, Bohari ya Dawa imezindua Bodi ya Usimamizi wa Kampuni Tanzu hiyo ambayo itakuwa na jukumu la usimamizi wa shughuli za uzalishaji wa bidhaa za afya. Hivyo, Kampuni hii itakuwa na uwezo wa kuingia ubia na wawekezaji wengine.

“Kwa sasa, kampuni hii itasimamia Kiwanda cha Mipira ya Mikono, Idofi – Njombe, Eneo la viwanda la Zegereni – Pwani, na Kiwanda cha Barakoa – Dar es Salaam. Kuongeza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani Serikali kupitia Bohari ya Dawa imeendelea kuongeza ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24, bidhaa za afya zenye thamani ya Shilingi bilioni 22.1 zilinunuliwa kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 14.1 mwaka 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 57.

“Dhamira hii itasaidia kuongeza uzalishaji na kuvutia wawekezaji ambapo matumizi ya fedha za kigeni yatapungua na ajira zitatengenezwa nchini,” amesema

USHIRIKISHAJI SEKTA BINAFSI

Mkurugenzi Mkuu huyo wa MSD, amesema katika kufanikisha azma ya Serikali ya kushirikisha sekta binafsi, Bohari ya Dawa imetambua maeneo yanayohitaji ushirikiano na sekta binafsi na inafanya uchambuzi ili wawekezaji wenye sifa waweze kushiriki kwenye uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya.

Aidha, Tukai alisema Bohari ya Dawa imekua ikifanya mawasiliano na balozi zetu zikiwemo Balozi za China, Korea Kusini, Urusi, Algeria na maeneo mengine duniani ili kuweza kufanya utambuzi wa wazalishaji, wawekezaji na kuwezesha ununuzi wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu kwa wazalishaji wa ndani.

“Uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya nchini Bohari ya Dawa ina viwanda viwili, ambavyo ni kiwanda cha barakoa kilichopo eneo la Keko, Dar es Salaam na kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi, Mkoa wa Njombe.

“Kwa upande wa Kiwanda cha kutengeza Barakoa, Keko Dar es Salaam, kinazalisha barakoa za kawaida na barakoa maalum (N95). Barakoa hizi hutumika kwenye matumizi mbalimbali ya kawaida kwa lengo la kujikinga na maambukizi au vihatarishi vinginevyo na pia hutumiwa na watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma nchini,”amesema

Amesema Kiwanda cha barakoa kimefanikiwa kuzalisha na kusambaza barakoa zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 4 na kufanya nchi kujitosheleza kwa uzalishaji wa barakoa.

MIKAKATI MWAKA WA FEDHA 2024/25

Akizungumzia mikakati ya mwaka wa Fedha 2024/25, Mkurgenzi huyo wa MSD amesema kuwa ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya na kuweza kujiendesha kibiashara ikiwamo kuwa na uwezo wa kifedha kupitia mtaji unaotolewa na Serikali, Bohari ya Dawa itafanya ununuzi wenye tija kutoka kwa wazalishaji na hivyo kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya.

“Kupitia Kampuni Tanzu, Bohari ya Dawa itaendelea na jitihada za kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya viwanda vya bidhaa za afya nchini hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

“Kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye Bima ya Afya ya Taifa na kuweza kutambua wahitaji zaidi wa bidhaa hizo nje ya MSD. Kutekeleza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Ruvuma, Arusha na Geita,” amessema

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here