Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametaja mambo manane ambayo serikali inakusudia kuyatekeleza ili kuhakikisha watu wenye ualbino wanalindwa.
Hayo ameyasema leo Juni 20, 2024 Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha tamko la Serikali kuhusu ulinzi wa mtoto kufuatia mauaji ya mtoto mwenye ualbino Asimwe Novart (2) wa kijiji cha Bulamula wilaya ya Muleba mkoani Kagera kuwa mambo hayo ni pamoja na;
I. Serikali inaandaa Mpango wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino (NAP) kwa kushirikiana na Chama cha Watu wenye Ualbino (TAS) na Wadau;
II. Serikali inaandaa kikao cha Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara kitakachofanyika tarehe 03 Julai, 2024 kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa watu wenye ualbino;
III. Kutoa elimu ya ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu wakiwemo Watu wenye Ualbino kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Elimu Maalum wa Mikoa yote nchini;
IV. Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na kuandaliwa kwa Mkakati wake wa Utekelezaji wa Miaka Mitano (National Five Year Implementation Strategy 2024/2025- 2029/2030) na Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miaka Mitano ambayo itazinduliwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025;
V. Kukamilisha na kuzindua Mkakati wa miaka mitatu 2024-2027 wa Upatikanaji wa Teknolojia saidizi kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino, mkakati huu umepangwa kuzinduliwa mwezi Julai, 2024;
VI. Kuandaa na kukamilisha Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu 2024/2025 – 2026/2027;
VII. Kuendelea na ubainishaji na usajili wa watu wenye ulemavu ngazi za kijiji na mtaa kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki na Kanzidata ya Watu wenye Ulemavu niliouzindua Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani tarehe 02 Desemba, 2023 jijini Dodoma.
VIII. Kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Watu wenye Ulemavu.