Home KITAIFA WAZIRI MKUU ATOA NENO UWEKEZAJI KILIMO CHA UMWAGILIAJI NCHINI

WAZIRI MKUU ATOA NENO UWEKEZAJI KILIMO CHA UMWAGILIAJI NCHINI

Google search engine

*AWATAKA WAKANDARASI KUTOA KIPAUMBELE  AJIRA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI, AMSHUKURU RAIS DK. SAMIA

* MNDOLWA AELEZA MIKATABA 24 ILIYOINGIWA IKIWAMO 14 YA UJENZI KWA KUTUMIA WAKANDARASI YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 248.7

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu na kuongeza bajeti.

Aidha amezielekeza Halmashauri zote nchini kuweka mpango mahsusi wa ardhi kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Majaliwa aliyasema hayo leo Aprili 30, 2024 Jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya umwagiliaji.

Alisema bajeti katika sekta ya umwagiliaji imeongezeka kwa asilimia 677 hadi kufikia Shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/2024 kutoka Shilingi bilioni 46.5 iliyotengwa kwa mwaka 2021/2022.

“Nitumie fursa hii kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan  kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya umwagiliaji nchini,”alisema

Aliongeza kuwa “Matarajio ya serikali ni kuona miradi inayotekelezwa itakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa ili kuwezesha kutimia kwa azma ya Serikali ya kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika Pato la Taifa kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030,”alifafanua.

MAAGIZO

Majaliwa aliwasisitiza Watendaji wote wanaohusika katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji wafanye kazi kwa ufanisi na wazingatie suala la uwazi pamoja na usimamizi mzuri wa fedha.

Alisisitiza kuwa fedha hizo ni kodi za wananchi wa Tanzania hivyo basi zitumike kuwanufaisha Watanzania wote.

“Wasimamizi wa miradi wahakikishe kuwa ubora wa miradi unalingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa kwenye miradi hiyo,” alisema.

Pamoja na hali aliwataka wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo inayotelekezwa kwa Force Akaunti wahakikishe wanatoa ajira kwa wananchi walio jirani na miradi hiyo.

“Wakandarasi na Wasimamizi wa miradi inayotekelezwa kwa force account, wahakikishe wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi walioko katika maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa na wahakikishe miradi inakamilika kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo,” alisema  

BASHE

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema mikakati ya serikali ni kuanza kutumia maji ya Ziwa Tanganyika katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji ambapo hatua ya kwanza itaanza katika mikoa ya Katavi na Rukwa.

Alisema baada ya Bunge la Bajeti kumalizika kutafanyika upembuzi wa kina na yakinifu ili maji hayo yasafirishwe hadi Simiyu ambapo kuna ukame na Tabora.

“Baada ya Bunge la bajeti kukamilika tunatarajia kuanza kuyatumia maji ya ziwa Tanganyika katika shughuli za kilimo na uzuri mitambo tunayo naamini Jambo hili litafanikiwa,” alisema

KAULI YA MNDOLWA

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Raymond Mndolwa alisema hafla hiyo ni kwa ajili ya utiaji sahihi wa mikataba 24 ambayo kati yake 14 ya ujenzi kwa kutumia wakandarasi yenye thamani ya Shilingi bilioni 248.7, miradi sita ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kutumia Washauri Elekezi yenye thamani ya Shilingi bilioni 9.35.

Alitaja miradi mingine minne itatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji yenye thamani ya sh.bilioni 16.95 ambayo itatekelezwa kwa utaratibu wa Force Account.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia ametoa fedha zaidi ya Shilingi bilioni 67 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji ambayo yatahudumia ekari zaidi ya 35,000.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here