Home KITAIFA NMB YAMWAGA MADAWATI, VITI, MEZA ZA MILIONI  33/- KWA SKULI TATU Z’BAR

NMB YAMWAGA MADAWATI, VITI, MEZA ZA MILIONI  33/- KWA SKULI TATU Z’BAR

Google search engine
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa (wa tatu kulia), akipokea sehemu ya msaada wa madawati 250 kutoka kwa Meneja wa Biashara wa NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (wa tatu kushoto). Madawati hayo yametolewa mwishoni mwa wiki kwa ajili ya wanafunzi wa skuli za msingi Uzini na Kidimni zilizopo katika jimbo la Uzini, Zanzibar. Wa pili kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ambaye pia ni Mbunge wa Uzini, Hamza Khamis Hamza. (Na Mpiga Picha Wetu)

NA MWANDISHI WETU

– ZANZIBAR

BENKI ya NMB imeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuboresha Sekta ya Elimu, baada ya kutoa msaada wa madawati 307 kwa Skuli tatu za msingi, pamoja na viti 100 na meza 100 kwa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume (KIST), vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni 33.

Katika hafla zilizofanyika Jumamosi Machi 9, 2024 kwenye maeneo na nyakati tofauti, NMB ilimkabidhi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhammed Mussa madawati 100 kwa ajili ya Skuli ya Uzini, madawati 150 ya Skuli ya Kidimni na mengine 57 ya Skuli ya Makadara, pamoja na viti 100 na meza 100 za KIST.

Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar,  Naima Said Shaame, ndiye aliyekabidhi misaada hiyo kwa Waziri Lela, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla zote kwenye Skuli za Kidimni na Makadara, kisha naye kuikabidhi kwa Walimu Wakuu wa Skuli hizo na Mkuu wa KIST papo hapo.

Awali NMB ilikabidhi madawati 250 kwa Skuli za Uzini na Kidimni na viti na meza kwa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume, makabidhiano yaliyoenda sambamba na ufunguzi wa madarasa, ofisi ya walimu, fremu za biashara na ukumbi wa mitihani wa Kidimni, zilizojengwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo la Uzini.

Madarasa, ofisi, fremu za maduka na ukumbi wa mitihani, zimeigharimu Ofisi ya Mbunge wa Uzini, Hamza Khamis Hamza ‘Chillo,’ kiasi cha Sh milioni 52.5, huku hafla ya pili ya makabidhiano hayo ikifanyika jioni katika Skuli ya Makadara, walikopewa madawati 57, sambamba na kuwazawadia wanafunzi waliofaulu michepuo.

Akizungumza katika hafla hizo, Waziri Lela aliishukuru NMB kwa kujali jamii kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI), na kwamba misaada hiyo imeiheshimisha Serikali yake, kwani inaenda kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kufundishia kwa walimu wa Skuli na chuo hicho.

“Tunawapongeza sana NMB na kuwashukuru kwa hiki mnachoendelea kukifanya katika skuli zetu na majimbo mengine yote nchini, mnatuheshimisha kwa sababu mnasaidia utekelezaji wa ilani ya chama chetu, mkiongoza taasisi zingine kuisaidia Serikali katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii.

“Mlitubeba pakubwa wakati wa janga la moto lililounguza skuli zetu hapa Zanzibar, leo mnakabidhi msaada mkubwa wenye thamani ya mamilioni ya shilingi. Fikisheni salamu zetu za shukrani kwa uongozi wa juu NMB kwa kutushika mkono kila tu.lipokuwa wahitaji,” amesema Waziri huyo.

Alibainisha ya kwamba NMB imesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule za jimbo lake na kuitaka kutowachoka kwani kadri idadi ya Wazanzibar inavyoongezeka, ndivyo changamoto katika sekta za elimu na afya zinavyoongezeka na hivyo Serikali kuhitaji nguvu za ziada kutoka kwa wadau.

Naima Shaame kwa upande wake alibainisha kuwa, changamoto za elimu ni kipaumbele kwa NMB, ambayo kupitia asilimia 1 ya faida yake kwa mwaka, imekuwa ikirejesha kwa jamii kupitia misaada ya madawati, viti, meza, kompyuta, vifaa vya kuezekea, ujenzi na ukarabati wa madarasa na ofisi.

“Leo Mheshimiwa Waziri tuko hapa kukabidhi madawati 250, viti na meza 100 kwa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume, ambako Skuli ya Uzini inapata madawati 100 na Skuli ya Kidimni madawati 150, huku KIST ikipewa viti 100 na meza 100, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni  33

“Tunaushukuru uongozi wa Jimbo la Uzini chini ya Mheshimiwa Hamza ‘Chillo,’ kwa kutambua umuhimu wa NMB kuwa ndio kimbilio lenu kwa changamoto zenu. Huu sio mwanzo na wala sio mwisho, tumefanya hivi mara nyingi na risala yenu inaonesha bado mna changamoto, nasi tunawakaribisha tena,”amesema.

Naima akawataka Wazanzibar uchangamkia fursa zitokanazo na ujio wa akaunti nafuu na raihisi isiyo na makato ya mwezi iitwayo NMB Pesa, ambayo inafunguliwa kwa Shilingi 1,000 tu, huku akiwataka kuwajengea watoto na wanafunzi visiwani humo utamaduni wa kujiwekea akiba tangu wakiwa wadogo.

Naye Naibu Waziri Hamza Chillo, aliishukuru NMB kwa jicho la huruma walilotumia kuiona Uzini kama sehemu sahihi ya kukabidhia misaada yao ya kielimu na kuwataka kutowachoka, badala yake wajiandae kuendelea kuwasaidia wakazi wa Jimbo lake katika kutatua changamoto za elimu ya Watoto wao.

Akitoa neno la shukrani, Dk. Khamis Khalid Said ambaye ni Naibu Mkuu wa Taasisi, Taaluma, Utafiti, Ubunifu na Ushauri Elekezi wa KIST, aliishukuru NMB kwa msaada wa viti 100 na meza 100 za wanafunzi, ambazo zitarahisisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia chuoni kwake.

“Kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, ambaye alipaswa kuhudhuria hafla hii, lakini akatingwa na majukumu, KIST inatoa shukrani za dhati kwa NMB kwa msaada huu mkubwa wanaotukabidhi, ambao nasi tutausafirisha kwenda Pemba tulikofungua ‘kampasi’ mpya ambayo haina fenicha muhimu kama hizi,” amesema.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here