Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
KLABU ya Waaandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, wamekubaliana na kufngua ukurasa wa ushirikiano katika kazi ikiwamo kumlinda mwandishi pindi anapokuwa kwenye majukumu hasa kwenye operesheni maalumu zinazohusisha jeshi hilo na makundi mengine.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika mjadala kuhusu usalama wa waandishi wa habari uliyoratibiwa na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, , Mtatiro Kitinkwi amesema jeshi hilo linathamini kazi kubwa inayofanywa na wanahabari katika kuibua taarifa mbalimbali kwa jamii.
“Jambo moja ni lazima kila pande itambue kwamba kwa sasa Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Jeshi IGP Camilius Wambura, limekuwa likifanya maboresho makubwa na hata leo kuwepo kwa mjadaa huo ni sehemu ya maboresho.
“Yapo ambayo sisi kama Jeshi tunaongozwa na sheria za Jeshi la Polisi ikiwamo na maagizo ambapo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida kabisa kwetu. Lakini kwa maana ya sasa tutaendelea kushirikiana nanyi kama wanahabari mna wajibu wa kuyasemea yale mazuri ya Jeshi lenu (Polisi) badala ya kuangalia mabaya tu.
“Sisi tupo tayari kushirikiana na hata tunapokuwa kwenye matukio maalumu tungependa kuwepo na utambulisho maalumu ili tuweze kuwatambua wanahabari kama njia ya kuwalinda ili waweze kutimiza majukumu yao kwa utulivu hasa tuwapo kwenye oparesheni maalumu,” amesema Kamanda Kitwinku
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Jeshi la Polisi litashirikiana na waandishi wa habari ikiwamo kutoa elimu ya namna ya kujilinda hasa kwenye oparesheni maalumu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa DCPC, Samson Kamalamo, amesema kuwa suala la ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari ni muhimu na kupitia DCPC itaendelea kuratibu hilo kama njia ya kumlinda mwandishi wa habari.
“Leo mjadala wetu unakweda kuliomba Jeshi la Polisi sasa limuone mwandishi wa habari kuwa si adui na nyakati zote hasa anapokuwa anatimiza majukumu yake Polisi asimuone kuwa ni adui na ana wajibu wa kumlinda ili aweze kutimiza majukumu yake,” amesema Kamalamo.
Akichangia mjadala huo, mwanachama wa DCPC Joseph Mwendapole, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na jeshi hilo huku akiomba elimu iendelee kutolewa kwa baadi ya askari hasa wa chini ili waone wana wajibu kwa jamii ikiwamo kutoa elimu kwa njia ambayo ni rafiki.