Home KIMATAIFA Waasi wa M23 wauteka mji wa mashariki mwa DR Congo

Waasi wa M23 wauteka mji wa mashariki mwa DR Congo

Google search engine

Wapiganaji wa kundi la waasi la M23 wameuteka mji wa Nyanzale kutoka kwa wanajeshi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

“Sasa tuko Nyanzale, adui amekimbia,” msemaji wa waasi Willy Ngoma aliambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu.

Kamanda wa Jeshi Jerome Chico Tshitambwe alithibitisha kwa shirika la habari la Reuters kwamba Nyanzale imetekwa na waasi.

Nyanzale, ambayo iko kilomita 130 (maili 80) kaskazini mwa mji wa Goma, ilikuwa ni kimbilio la watu waliotoroka makazi yao kutokana na mapigano katika maeneo jirani.

Lakini mapema wiki hii maelfu ya watu walitoroka tena Nyanzale iliposhutumiwa.

Ngoma amesema kwa sasa wengi wamerejea mjini.

Isaac Kibira, Naibu wa Gavana katika mji wa karibu wa Bambo, amesema M23 walikuwa wakifyatua risasi “kiholela” kabla ya kuuteka Nyanzale.

“Tulishuhudia kutekwa kwa Nyanzale na M23 tangu asubuhi na idadi ya waliofariki iliongezeka hadi 15,” Kibira ameiambia Reuters.

Kundi la M23, lililoundwa kutokana na kundi lingine la waasi lilianza kufanya kazi mwaka 2012 – kwa kiasi kikubwa kulinda wakazi wa eneo la Watutsi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia mateso na ubaguzi.

Wapiganaji wake walichukua silaha tena mwaka wa 2021, wakilalamikia kuvunjwa kwa ahadi katika mkataba wa amani wa awali.

Wapiganaji wa M23 wana vifaa vya kutosha, lakini kundi hilo linakanusha kuwa wakala wa Rwanda.

Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulisema “unasikitishwa sana na kuongezeka kwa ghasia” na kutoa wito wa mazungumzo kati ya DR Congo na Rwanda ili kukabiliana na chanzo cha mzozo huo.

CHANZO: BBC

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here