Home KITAIFA TUME YA MADINI YAENDELEA KUTOA ELIMU USHIRIKISHWAJI  WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI...

TUME YA MADINI YAENDELEA KUTOA ELIMU USHIRIKISHWAJI  WATANZANIA KATIKA SEKTA YA MADINI CHUO CHA MIPANGO

Google search engine

*Wadau wa elimu washauriwa kushirikiana na vyuo vya nje kwenye teknolojia,  Wahadhiri wabaini  fursa kwenye eneo la wajibu wa kampuni za madini  kwa jamii (CSR)

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

IKIWA ni moja ya mikakati ya kuhakikisha wadau wanabaini fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na kushiriki.

Kutokana na hali hiyo Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini leo Machi 7, 2024 imeendelea kutoa mafunzo kwa wahadhiri wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kilichopo jijini Dodoma kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Afisa Biashara wa Madini kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini, Issa Lunda ameshauri wadau wa elimu kushirikiana na vyuo vya nje kwa kubadilishana uzoefu na teknolojia mpya hasa katika eneo la madini na kuingiza elimu mpya kwenye mitaala na kuzalisha wanafunzi bora watakaoweza kuajiriwa kwenye migodi ya madini nchini.

“Ikiwa ni utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kunadi fursa zilizopo katika migodi ya madini, ni vyema vyuo vya elimu vikawekeza kwenye teknolojia ya kisasa hasa kwenye uendeshaji wa mitambo kuanzia kwenye utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini kwa kubadilishana uzoefu na maarifa na vyuo vya nje na kuzalisha wataalam watakaoweza kuendana na mahitaji ya soko la ajira kwenye migodi ya madini,” amesema Lunda.

Akielezea namna vyuo vya elimu vinavyoweza kushiriki kwenye migodi ya madini Lunda amefafanua kuwa katika migodi ya madini zipo fursa kama  vile usambazaji wa vifaa kinga, mitambo ya utafiti na uchimbaji wa madini, usafiri kwa wafanyakazi wa migodi, ujenzi wa majengo, uchorongaji na ushauri uelekezi wa namna ya kusimamia migodi ya madini na kushauri vyuo kuweka nguvu katika wanafunzi wanaoweza kuwa wataalam baadaye na kutoa huduma katika migodi ya madini.

Awali akielezea mchango wa kampuni za madini kwa jamii, katika mafunzo hayo Meneja wa Ukaguzi wa Kodi, Fedha na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Annasia Kwayu amesema kuwa kampuni za madini zimeendelea kuboresha huduma za jamii kama vile ujenzi wa vituo vya afya, shule, maji safi na maboresho  ya miundombinu sambamba na kuwawezesha wananchi kwenye miradi.

“Mfano mzuri ni Mgodi wa Dhahabu wa Shanta ambao umewawezesha wananchi katika eneo la Songwe kwa kuwapatia mbegu za ufuta na mafunzo ambao wameanza kulima na kuuza mazao yao nje ya nchi na kupata fedha za kigeni  huku Serikali ikipata kodi yake,”amesema Kwayu.

Akielezea lengo la kutoa mafunzo katika Taasisi za elimu Kwayu amesisitiza kuwa ni mkakati wa kuhakikisha wadau wa elimu wanafahamu fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na kuzalisha watalaam wenye sifa zinazoendana na soko la ajira na bidhaa kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

“Lengo letu kama wataalam kutoka Tume ya Madini ni kuhakikisha tunasambaza elimu kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Madini kwa wadau wa madini nchini katika sekta zote watakaoweza kujiajiri kupitia utoaji wa huduma muhimu kwenye migodi ya madini kama vile utoaji wa ushauri wa kifedha, vyakula, ulinzi na kujipatia kipato huku Serikali ikikusanya mapato yake yanayotokana na kodi mbalimbali,” amesema Kwayu.

Ameendelea kusema kuwa elimu ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini itaendelea kutolewa kwa wadau wote wa madini nchini kuanzia kwa wananchi wanaoishi jirani na migodi ya madini, watendaji kuanzia kwenye ngazi za vijiji, kata,  wilaya, mikoa, watoa huduma kwenye migodi ya madini na wananchi wote ili kuongeza uwekezaji wa wananchi kwenye Sekta ya Madini.

“Tunaamini  ongezeko la  ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini litaendelea kufanya mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kuendelea kukua kwa kasi sambamba na ukuaji wa Sekta ya Madini,” amesisitiza Kwayu

Wakati huohuo akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Idadi ya Watu kutoka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Dk. Richard Mgabo sambamba na kutoa pongezi kwa Tume ya Madini kwa mafunzo hayo, amesema kuwa Chuo kimebaini fursa kubwa hasa kwenye eneo la Wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR) na kuongeza kuwa chuo kipo tayari kuwasaidia wananchi kufahamu na kubuni miradi ambayo ni endelevu hasa baada ya kumalizika kwa uchimbaji wa madini.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here