Home KITAIFA SERIKALI, WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO WAINGIA MAKUBALIANO KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO NCHINI

SERIKALI, WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO WAINGIA MAKUBALIANO KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO NCHINI

Google search engine

*NI MKATABA WA GHARAMA YA SHILINGI BILIONI 50

Na INNOCENT MUNGY

 -DAR ES SALAAM

KATIKA hatua muhimu kwa Sekta ya Mawasiliano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano ya maridhiano na watoa huduma wa mawasiliano yenye thamani ya Shilingi bilioni 50 kama malipo ya matumizi ya miundombinu tangu kujengwa kwake.

Aidha, watoa huduma hao wameahidi pia uwekeza Sh bilioni 32.5 katika maendeleo ya miundombinu zaidi nchini.

Serikali imefikia makubaliano hayo ya kihistoria na watoa huduma hao wa mawasiliano nchini katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo Septemba 25, 2023 katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na watoa huduma wa mawasiliano nchini ambapo makubaliano hayo yanalenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na yamejumuisha kampuni kubwa za simu za Airtel Tanzania, Honora Tanzania (Tigo), na Vodacom Tanzania.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza Sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi wa Tanzania.

 Waziri Nnauye alimshukuru, Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujitolea kwake kukuza Sekta ya Mawasiliano.

Waziri Nape amesema kuwa dhamira ya serikali kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote na kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, Nape, amewapongeza viongozi wa serikali walioshiriki katika majadiliano na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya mawasiliano nchi ili kufikia uchumi wa kidijitali.

 Makubaliano hayo ya kihistoria yalianzishwa mnamo Oktoba 4, 2011 yalilenga kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa mkongo wa taifa katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma ya mawasiliano.

Katika hafla hiyo ya utiaji saini, watoa huduma wa mawasiliano walikubaliana kutoa dola milioni 20 kwa matumizi ya kipindi cha miaka mitano na kuahidi kuwekeza Dola za Marekani milioni 13 katika maendeleo ya miundombinu zaidi.

Hafla hiyo pia ilishuhudia kujiunga kwa Vodacom Tanzania kama mwanachama wa muungano huo, ikionyesha ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali katika kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi na kukuza uchumi.

Serikali imedhamiria inafikia lengo la kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia Watanzania wote na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali, na inalenga kufikia asilimia 85 ya Watanzania wenye ufikiaji wa intaneti ya kasi ifikapo mwaka 2025.

 Aidha Waziri Nnauye alitoa maelekezo ya utekelezaji wa makubaliano haya na kuwasihi watoa huduma wa mawasiliano kuendelea kuwekeza katika miundombinu ili kufikia wananchi wengi zaidi. Hafla hii ilipokelewa kwa furaha kutoka pande zote mbili na inaonyesha hatua muhimu kuelekea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini Tanzania.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here