Home KITAIFA RAIS DK. SAMIA SULUHU HASSAN AHIMIZA USTAARABU KATIKA SIASA

RAIS DK. SAMIA SULUHU HASSAN AHIMIZA USTAARABU KATIKA SIASA

Google search engine
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa domorasia jijini Dar es Salaam

NA MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kile kilichoonekana kama kukerwa na mwenendo wa baadhi ya Wanasiasa nchini amesema kutamka yasiyofaa hadharani ni kukosa malezi.

Aidha amesema ni ‘umajununi’ unaoakisi kudhoofika kwa afya ya akili kwa wale wasio na haya ambao ndimi zao hutoa lugha chafu kwa dhana ya kujinufaisha kisiasa.

Amesema Watanzania wana mila na desturi zenye staha na ustaarabu zinazotiwa nguvu na mafunzo ya dini zao mbali ya elimu wapatazo kwenye mifumo rasmi ya elimu.
“Yule ambaye haoni haya kutoa kauli chafu dhidi ya wengine tena hadharani, huyo amekosa malezi ya kidini”, ameasa Rais Samia akizungumza katika mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa jumatatu wiki hii.

Amesema alitegemea fursa iliyotolewa kwa Vyama kufanya mikutano ya siasa ingetumika kujiimarisha kwa Vyama hivyo kwa kunadi sera mbadala na chama tawala ili wananchi waweze kuviamini.

Hata hivyo, amesema katika hali ya kushangaza fursa hiyo imekuwa ikishuhudia utoaji matusi, kushambulia watu na kufanya uchochezi unaolenga kuvuruga amani.

“Hakuna mwenye kifua cha kuvumilia, hata hivyo kumkimbiza mwehu aliyepora nguo … wote mtaonekana wendawazimu”, ameasa.

Amesema miaka michache iliyopita, vyama havikuweza kufanya mikutano, aliamua kuruhusu ili kuimarisha demokrasia nchini, hata hivyo amesema inasikitisha kuona wengine wakitumia vibaya fursa hiyo kwa kutoa maneno machafu.

“Wamekuwa wakidandia, mara Katiba, mara Bandari, hii inaonyesha hawana la kuwaambia wananchi ndio maana wanazungumza yasiyostahiki, kinywa cha mtu aliye na malezi ya kidini hakiwezi kutoa kauli zisizo staha katika jamii”, ameonya.

Katika siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama na wanaharakati wengine wameripotiwa kurusha maneno makali dhidi ya Serikali kwa ujumla lakini dhidi ya Rais Samia kwa namna ya pekee kupitia majukwaa ya kisasa na vyombo vya habari.

Wamekuwa wakitoa shutuma, vitisho na kejeli dhidi Serikali katika kile kinachodaiwa kama kutoa maoni yao kuhusu masuala ya Katiba na Mkataba wa Uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here