Home KITAIFA Michezo ya kubashiri ‘yavunja ndoa’ Wilayani Ikungi

Michezo ya kubashiri ‘yavunja ndoa’ Wilayani Ikungi

Google search engine
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Ally Mwanga (katikati) akiongoza kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu kuanzia kilichoketi wilayani humo Mei 19, 2023. Kushoto ni Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovson Mtangeki na kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Justice Kijazi.

Na Dotto Mwaibale, Ikungi

ONGEZEKO kubwa la vijana kushiriki michezo ya kubashiri (Kubeti), limedaiwa kusababisha ndoa kuvunjika na kukithiri kwa uhalifu katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.     

Hayo yamesemwa na Diwani wa Kata ya Mtunduru, Ramadhan Mpaki wakati akichangia kwenye Kamati ya Fedha na Uongozi katika kikao cha baraza la madiwani cha robo tatu kuanzia Januari hadi Machi 2023 kilichoketi Mei 19, 2023 wilayani humo.

Mpaki amesema kwa siku za karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya ndoa kuvunjika na uhalifu kuongezeka na sababu kubwa ni kutokana na vijana kujihusisha na michezo ya kubashiri.

Diwani huyo amesema iwapo hakutakuwa na hatua za haraka kudhibiti michezo ya kubashiri ni wazi kuwa hali itazidi kuwa mbaya, kwa ndoa kuvunjika na uhalifu kuongezeka.

Mpaki ametoa ushauri kwa baraza la madiwani kuangalia namna ambayo inaweza kufikisha jambo hili katika  mamlaka za kutunga sheria ili ziweze kuona namna ya kulitatua, kwani hali ni mbaya kwa sasa hasa kwa wanandoa.

“Naomba halmashauri yetu iangalie upya sheria ya mchezo huu wa kubashiri, kwani pamoja na kuwa chanzo cha mapato vijana wamekuwa wakicheza mchezo huo hadi usiku wa manane ambapo pia wamekuwa wakipanga vitendo vya kufanya uhalifu ikiwa ni pamoja na kutishia ndoa za watu,” amesema Mpaki bila ya kufafanua.

Aidha diwani huyo amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukasanyaji wa mapato, huku wakizingatia misingi ya utawala bora.

Naye Diwani wa Kata ya Mwaru, Iddi Makangale amempongeza Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Mwanga na Mkurugenzi, Justice Kijazi kwa mafanikio inayopata wilaya hiyo chini ya uongozi wao kwa kushirikiana vizuri na watendaji wa kata, tarafa na wataalamu.

Pia Makangale amezipongeza kata za Mgungila, Mwaru na Mkiwa kwa kuongoza kwa kukusanya mapato na kuzitaka kata zingine kuiga mfano huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ally Mwanga amewataka watumishi wote na viongozi kuwa wazalendo na kushirikiana ili kuiletea maendeleo wilaya hiyo.

Mwanga amesema suala la ukusanyaji wa mapato ni la kufa na kupona na akasisitiza uzalendo katika jambo hilo na kuwa uhai wa halmashauri yoyote unatokana na mapato na si vinginevyo.

Kwa upande wake Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Dijovson Mtangeki, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson aliipongeza halmashauri hiyo kwa kupata hati safi kwa miaka tisa mfululizo na kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa kada zote za utumishi wakiwamo madiwani na Serikali.

Amesema halmashauri hiyo imekuwa na miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha na kuwa kazi ya ukaguzi ni lazima ifanywe na viongozi wote na si kumuachia mkuu wa wilaya peke yake.

Amesema licha ya kuwepo kwa kamati, wataalam, maofisa kata na tarafa kwa ajili ya kusimamia miradi hiyo katika utekelezaji wake madiwani hawawezi kukwepwa kwa namna yoyote ile ukizingatia kuwa miradi mingi inayofanyika ipo kwenye maeneo yao.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nimesimama mbele ya baraza lako hili tukufu kuwaomba madiwani wetu walau wawe wanakwenda kuikagua miradi hiyo mara mbili kwa wiki watakuwa wamesaidia kwani nguvu yao inahitajika sana,” alisema Mtangeki.

Aliwaomba madiwani hao kuilinda,kuisimamia na kuwahamasisha wananchi waweze kushiriki katika utekelezaji wake na itekelezwekwa wakati na viwango vinavyohitajika.

Katika hatua nyingine Mtangeki ameomba wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo vitu vinavyosaidia ujenzi kama mchanga, mawe na vingine vifikishwe eneo la ujenzi siku moja kabla tofauti na ilivyo sasa ambapo huwa vinapelekwa siku ya kazi jambo ambalo linawafanya mafundi wasifanye kazi kwa ufanisi.

Akizungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Justice Kijazi amesema mwaka wa fedha wa 2023/ 24 madiwani wote wa halmashauri hiyo watafanya ziara ya mafunzo kwenda Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kujifunza namna bora ya utunzaji wa mazingira kutokana na wilaya hiyo kuwa kinara wa utunzaji mazingira hapa nchini.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kuibuka kwa hoja za madiwani kutaka kufnyika kwa ziara ya mafunzo ya namna bora ya utunzaji wa mazingira.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here