Na Mwandishi Wetu
-Dar es Salaam
Aliyekuwa Mwenyekiiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Wananchi CUF (JUKE), ambaye pia alikuwa Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge la la 10, Kiza Mayeye nimejiondoa kwenye Chama hicho na kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo.
Kwa mujibu wa tamko alilolitoa leo mkoani Dar es Salaam kwa waandishi wa habari Mayeye, amesema kuwa pamoja na na kuchukua uamuzi huo pi ameshajiandikisha katika mfumo wa chama hicho wa kieletroniki.
“Nimekwishajisajili kwenye mfumo wa kuandikisha wanachama wa ACT Kiganjani, nimelipia aina ya kadi ya Maalim Seif na ada ya uanachama kwa miezi sitini (miaka mitano). Hivyo mimi ni mwanachama kamili wa ACT Wazalendo
“Nimekitumikia Chama cha CUF kwa nafasi mbalimbali tangu mwaka 2011 nilipojiunga nacho. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipokishukuru Chama cha CUF kwa kunilea kiuongozi na kunipa fursa mbalimbali kukitumikia.
“Leo, nimelazimika kuchukua maamuzi haya magumu kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika. Mosi, mimi ni mwanasiasa wa vitendo. Naamini siasa halisi ipo chini (field), kwa wananchi. Mwaka 2020 niligombea Ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini na kwa matokeo halisi nilishinda lakini kilichotokea mwaka 2020 sote tunakifahamu,” amesema Mayeye
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa mwaka 2020 walioshinda walishindwishwa na walioshindwa walishindishwa!
Amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipotangaza kuwa amekuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 16,252 kila mmoja alishangaa
“Bila shaka hata CCM wenyewe walishangaa, kwa sababu walijua nilishinda!. Ninajiunga ACT Wazalendo ili kuendeleza mapambano. Nimefanya uchambuzi wa kina na kujiridhisha kuwa ACT Wazalendo ndio jahazi sahihi la kuendeleza harakati zangu kwa ajili ya kuwakomboa wanachi wa Kigoma Kaskazini, Mkoa mzima wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
“Nimevutiwa sana na sera za ACT Wazalendo za kujenga Tanzania ya wote kwa maslahi ya wote. Nimeshawishika pia na jitihada za Chama kuimarisha mtandao wake nchi nzima. Nimevutiwa pia na jitihada za Chama kukuza vipaji vya vijana na wanawake,” amesema
Kiongozi huyo amesema kuwa kabla hajafanya uamuzi huo alizungumza na vyama vingi ili kufanya utafiti kabla ya kujiunga na chama husika.
“Mwishowe nikafanya hitimisho kuwa ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi. Wale ambao walitarajia nitajiunga nao, waniwie radhi, vigezo vya kisayansi vimenipeleka ACT Wazalendo.
“Nimekuja kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa Chama katika kujihakikishia ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025. Ninatarajia kwenda Jimboni Kigoma Kaskazini hivi karibuni, huko nitaeleza kwa kina
zaidi kwa nini chama hiki kinapaswa kuwa tumaini lao kutokana na utafiti na uchambuzi wa kina nilioufanya,” amesema