Home KITAIFA Chalamila atua Dar kwa kishindo, aanza ziara abaini mazito kwa TRA

Chalamila atua Dar kwa kishindo, aanza ziara abaini mazito kwa TRA

Google search engine

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akisalimiana na mmoja wa askari Polisi katika Soko la Mwenge
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akizungumza na wafanyabishara katika Soko la Mwenge

Na Mwandishi Wetu

-Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametua jijini hapa na kuanza kazi kwa kishindo ikiwamo kufanya ziara  katika Soko la Mwenge lililopo Manispaa ya Kinondoni na kubaini mazito.

Katika ziara hiyo aliyofanya leo baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam, akitokea Mkoani Kagera, ikiwa siku moja tangu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipotangaza kufanya mabadiliko madogo ya wakuu wa mikoa minne.

Katika mabadiliko hayo yalifanywa jana Chalamila amehamishiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam akichukua nafasi ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla ambaye amehamishiwa Mkoa wa Mwanza kuendelea na majukumu hayo.

Akizungumza na wafanyabishara katika Soko la Mwenge, RC Chalamila, amesema kuwa hatua yake ya kupita kwenye maduka mbalimbali mkoani hapa ni kujionea hali halisi ya kinachozungumzwa na wafanyabiashara ambao siku ya jana walilazimika kugoma kutokana na kile wanachodai kupinga tozo za kodi lukuki zinazotozwa na TRA.

“Pamoja na kuwa sijaingia ofisini rasmi lakini nimeona ipo haja ya kusikia hasa huku mtaani watu wanasema nini, lakini katika moja eneo nililopita watu wanalalamikia uwepo wa kodi kubwa zisizoweza kulipwa na wafanyabiashara kutokana na kiwango kikubwa cha VAT ambayo ni asilimia 18,” amesema Chalamila.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa, amesema kuwa suala lingine ambalo linalalamikiwa na wafanyabiashara hao ni kuhusiana na Idara ya Forodha ambayo imeweka viwango vikubwa vya kodi hasa katika vitenge pamoja na mlolongo mrefu wa ufuatiliaji ambapo ni kikwazo kwa wafanyabiashara wengi.

“Jambo la tatu ambalo nimelisikia ni kuwepo kwa zoezi la kamata kamata kwa Wafanyabiashara Kariakoo na kuwakosesha uhuru pamoja na kuleta usumbufu kwa wateja wao na hasa kwa wateja  wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zambia, Malawi pamoja na mataifa mengine,” amesema RC Chalamila.

Pia mkuu huyo wa mkoa amesema  kuwa jambo linguine alilobaini kwa wafanyabiashara katika eneo la Mwenge ni kuwepo kwa wafanyakazi  ambao ni wanafunzi huku akidai kwamba wamekuwa wakitumiwa na Mamlaka ya Mapato  Tanzania (TRA) ambao wanakuwa hawana uwezo wa lugha nzuri na yenye staha kwa wafanyabiashara.

“Jambo lingine ni utaratibu wa TRA kuruhusu mizigo kutoka Bandarini na baadae tena Wanakuja Kukagua nyaraka Sehemu za Kuhifadhia Mizigo (Godown), jambo ambalo wafanyabiashara wanasema ni Usumbufu mkubwa kwao”

“Kubwa zaidi ni kauli ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kusamehe kodi ya miaka mitatu au mitano nyuma, ambapo wafanyabiashara hawajaweza kuichukua kauli ya Rais kwa vitendo, ambao sasa TRA wamekuwa wakiomba barua rasmi kutoka kwenye mamlaka hizo kwa maana ya Rais, Waziri Mkuu au Makamu wa Rais” amebainisha RC Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akiondoka kwa usafiri wa Bajaj katika Soko la Mwenge baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wafanyabishara
Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here