Home KITAIFA Mkurugenzi JATU amwangukia DPP kukiri makosa

Mkurugenzi JATU amwangukia DPP kukiri makosa

Google search engine

NA MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mkuu wa Kampuni ya JATU PLC, Peter Gasaya (33) anayekabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujipatia Sh.Bil 5.1 /- kwa njia ya udanganyifu, amemwandika barua ya kukiri na kuomba apunguziwe adhabu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP).

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya JATU kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa huyo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Aprili 24, 2023 mbele ya hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo Richard Kabate, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mkurugenzi Jatu akamatwa tena
Kitaifa 3 hours ago
Gasaya, kupitia wakili wake, Nafikile Mwamboma amedai kuwa ameandika barua kwa DPP, tangu Aprili 20, 2023 akiomba kukiri mashtaka yake ili aweze kuimaliza kesi hiyo.

Awali, kabla ya mshtakiwa huyo kudai kuwa amemwandikia barua DPP, Wakili wa Serikali Ashura Mnzava alidai kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake haujakamilika.

Wakili Mnzava baada kueleza hayo, ndipo mshtakiwa huyo, alipoieleza mahakama kuwa ameandika barua kwa DPP ya kukiri mashtaka yake ili aweze kuimaliza kesi hiyo.

Hakimu Kabate, baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, ametoa siku 30 kwa ajili ya mshtakiwa na upande wa mashtaka kukutana na kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.

Hakimu Kabate baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 8, 2023 kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video huku mshtakiwa akiwa rumande katika gereza la Keko.

Mshtakiwa huyo yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, katika ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5,139,865,733 kutoka Saccos ya JATU.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka Saccos ya JATU kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika Jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo ya tukio, akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa JATU SACCOS, alijihusisha na muamala wa Sh 5,139,865,733 kutoka katika akaunti ya JATU SACCOS iliyopo Benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya JATU PLC liyopo katika Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here