Home KITAIFA Kinara wa kuzalisha, kusambaza dawa bandia za binadamu atiwa mbaroni jijini Dar...

Kinara wa kuzalisha, kusambaza dawa bandia za binadamu atiwa mbaroni jijini Dar es Salaam

Google search engine

NA MWANDISHI WETU,
DAR ES SALAAM.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki imefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu wa kuzalisha na kusambaza dawa bandia za binadamu Bw William Japhet Mwangile mkazi wa maeneo ya Matembele Lodge Kipunguni Kata ya Kipawa, Ilala, Dar es Salaam.

Mtuhumiwa huyo amekuwa akitafutwa na TMDA tangu mwezi Machi, 2023 kufuatia kukamatwa kwa baadhi ya dawa anazodaiwa kuzizalisha na kuzisambaza pamoja na watu aliokuwa anashirikiana nao katika usambazaji.

Akielezea katika eneo la tukio, Mkaguzi wa Dawa wa TMDA Kanda ya Mashariki, Japhari Mtoro amesema kuwa:

TMDA ilikuwa inamtafuta mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za kuzalisha na kusambaza dawa hizo banda zikiwa zimefungashwa kwenye makopo kinyume cha kifungu cha 76 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219.

“Mtuhumiwa amepatikana April 14, 2023 mchana kufuatia taarifa za kiinteligensia na mtego uliokuwa umewekwa na vyombo vya dola.

Mara baada ya kumkamata, TMDA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali za mitaa, tumefanya upekuzi nyumbani kwake maeneo ya Matembele na nyumbani kwa wazazi wake maeneo ya Kitunda relini ” Amesema Japhari Mtoro

Ambapo amebainisha kuwa, vitu mbalimbali vinavyohusiana moja kwa moja na tuhuma zinazomkabili vimepatikana.

“Nyumbani kwake tulibahatika kupata lebo 537 za ambazo zimekwishachapishwa taarifa za dawa(printed labels) mfano Quinine Sulphate, Erithromycin, Ampiclox, Paracetamol.

Lakini pia tulikuta Makopo 12 matupu ambayo hutumika kufungasha dawa,

Pia tulikuta viroba vitatu , kiroba kimoja Unga wa njano na viwili unga mweupe unaodhaniwa kuwa ndizo malighafi zinazotumika kutengeneza dawa hizo.” Amesema Japhari

“Lakini pia kwa upande wa nyumbani kwa wazazi wake tumefanikiwa kukamata jumla ya lebo 142 zilizokwishachapishwa taarifa za dawa na kufanya jumla ya lebo zilizokamatwa kuwa 679, vilevile, tumekuta virobo viwili vyenye kapsuli za dawa aina ya Ampiclox zikiwa hazina kitu.

Mtuhumiwa huyu ataunganishwa na wenzake waliokwisha kukamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya Sheria ili waweze kuwajibika na tuhuma zinazowakabili.

Japhari amesema tukio hilo ni la uhalifu dhidi ya binadamu kwani ni la unyama na ukatili wa hali ya juu kwani mtu anazalisha dawa bandia, dawa ambazo pengine hamna kitu humo ndani, mtu anatumia dawa anategemea atapona, lakini anakutana na dawa bandia zinazoweza kusababisha mtu kupoteza maisha.

“Lakini pia nitumie fursa hii kuwashukuru sana wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa serikali ya mtaa, Jeshi la Polisi, na wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa uliofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu” amesema Japhari.

Kwa upande wake Mary Grogory Mambo ambaye ni Mjumbe wa shina namba 6 mtaa huo wa Matembele ya kwanza maarufu Matembele Lodge, aliyekuwa akishirikiana na TMDA na jeshi la Polisi kwenye upekuzi huo, ameomba wananchi waendelee kushirikiana kutoa taarifa kwa TMDA kufichua hali kama hiyo ya watu wanaofanya ama kutengeneza dawa bandia.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here