Home KITAIFA Waziri Mkuu awataka Viongozi wa Dini kuhimiza maadili mema, kukemea unyanyasaji jinsia...

Waziri Mkuu awataka Viongozi wa Dini kuhimiza maadili mema, kukemea unyanyasaji jinsia nchini

Google search engine
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waumini na viongozi wa Dini ya Kiislamu alipomuwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika mashindano ya Quraan yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aisha Sururu, katika Ukumbi wa Dimond Jubilee jijini Dar es Salaam
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir Bin Ally wa Mbwana, akizungumza katika mashindano ya kuhifadhi Quraan yaliyoandaliwa na taasisi ya Aisha Sururu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi mshindi wa kwanza wa kuhifadhi Quraan Juzuu (30) upande wa wavulana, Mussa Hamad, namba za usajili wa pikipiki ya kubebea mizigo baada ya kuibika mshindi.
Mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa akimkabidhi mshindi wa pikipiki wa kuhifadhi Koran Juzuu (30) baada ya kuibkuka mshindi wa pili katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya Aisha Sururu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini kila wanapopata nafasi kwenye mimbari wakemee kuhusu ukatili wa kijinsia pamoja na wale wanaoenda kinyume na maadili na desturi za Kitanzania.

 Ametoa wito huo leo Jumapili, Aprili 2, 2023) wakati akizungumza na viongozi na waumini waliohudhuria mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo yaliandaliwa na taasisi ya Aisha Sururu Foundation (ASF).

“Nitoe rai kwa viongozi wetu wa dini muendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda mila, desturi na tamaduni za Kitanzania hususan katika kipindi hiki tunachokabiliwa na wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili,” amesema.

“Sasa hivi Tanzania inakabiliwa na tatizo la mmomonyoko wa maadili na pia kumeibuka wimbi la vitendo vingine ambavyo vinakwenda kinyume kabisa na dini zetu pamoja na mila, desturi na tamaduni za kitanzania. Ninampongeza sana Dk Aboubakar bin Zubeir, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania kwa kulisimamia kidete suala hili ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo mahsusi kwa viongozi wote wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania kulikemea na kutolifumbia macho.”

Amesema licha ya kukithiri kwa vitendo hivyo vya mmomonyoko wa maadili, Waislamu wanajivunia uwepo wa Quran tukufu ambayo katika sura ya 33 aya ya 21 (Quran 33:21) wanakumbushwa kwamba wanacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. “Kwa lugha nyingine Quran inapaswa kuwa chanzo cha kutegemewa cha mafunzo sahihi ya tabia njema, utii na kuheshimu mamlaka zilizopo,” amesisitiza.

“Tunapowahifadhisha Quran vijana wetu, tuhakikishe jambo hilo jema linakwenda sambamba na ujenzi wa misingi imara ya malezi itakayowafanya wawe raia wema, waadilifu na wazalendo kwa nchi yao. Tukiwa wazazi, walezi na walimu wa Quran, nitoe rai kwamba tunapotoka hapa hebu tujiulize ni kwa kiasi gani tunaizingatia hii Quran tukufu katika mwenendo mzima wa maisha yetu ya kila siku.”

Waziri Mkuu amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wanamsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye mara zote amekuwa akiguswa na suala zima la maadili hususan kwa vijana.

“Pia tutamsaidia Rais kupata wasaidizi wacha Mungu na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba waumini hao waendelee kuiombea amani Tanzania kwani ikipotea mikusanyiko kama hiyo haifanyika.

“Nasi tuendelee kuiombea nchi yetu na viongozi wake ili waendelee kuliongoza vema Taifa letu ikiwa ni pamoja na kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii,” amesisitiza.

Amesema Quran sura ya pili aya ya 126 (Quran 2:126) inawakumbusha umuhimu wa kuiombea nchi amani kupitia dua ya Nabii Ibrahimu alipouombea mji wake na wakazi wake amani na neema.

Mapema, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dk. Zubeir amempongeza Mwenyekiti wa taasisi ya ASF, Sururu kwa kuandaa mashindano hayo kwa miaka 22 na kumueleza kwamba ni mwanamke pekee Tanzania na Afrika Mashariki ambaye anafanya kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Amana ambao ni wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Aboubakar Ally amesema kwa mwaka huu wametenga sh. bilioni 40 kwa ajili ya uwezeshaji wa vikundi na wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

Akisoma risala ya ASF, Zainab Matitu Vulu amesema washiriki wa mashindano hayo wanatoka maeneo tofauti nchini ambao jumla yao walikuwa 600 kutoka mikoa 20 ya Tanzania bara na visiwani na baada ya mchujo waliofanikiwa kuingia fainali ni 77.

Aliyataja baadhi ya majukumu yao ni kuwaunganisha vijana wa shule za sekondari na vyuo vikuu, kutoa ufadhili kwa baadhi ya vijana, kuwafundisha stadi za maisha na kuwasaidia wajane.

Amesema wana kiwanja walichonunua ambacho kipo Kiparang’anda wilayani Mkuranga, lakini wanahitaji fedha za kujenga chuo cha kuwafundisha vijana stadi za maisha na kuwahifadhisha Quran tukufu

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here