Home KITAIFA Ujenzi SGR Mwanza-Isaka wafikia 28%

Ujenzi SGR Mwanza-Isaka wafikia 28%

Google search engine

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

UJENZI wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tano kinachoanzia Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga umefikia asilimia 28.

Meneja wa mradi huo, Christopher Kalisti, aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC) waliotembelea mradi huo eneo la Fella, Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza.

Alisema mradi huo utakamilika ndani ya muda kulingana na mkataba ambapo ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa Kilometa 342 unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya sh. trilioni 3.06 na utakamilika Mei, 2024.

“Serikali inatekeleza mahitaji muhimu ikiwemo malipo ya fedha, hadi kufikia Februari 28, 2023 Mkandarasi alikuwa ameshalipwa zaidi ya sh. bilioni 700.

“Tayari mataruma ya reli yameanza kutandazwa katika eneo lenye urefu wa Kilometa nne, tunaamini mradi huu utakamilika kwa mujibu wa mkataba,” alisema.

Kuhusu huduma kwa wafanyakazi, alisema uongozi unatoa huduma bora za msingi ikiwemo chakula, malazi na usalama kazini.

Lengo ni kuongeza ari ya kazi, kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kikamilifu ili kukamilisha mradi kwa wakati.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa PIC, Jerry Silaa alisema kamati yake imeridhishwa na mwenendo wa utekelezaji mradi huo akiwataka wananchi waishio maeneo jirani kutumia fursa hiyo kujiimarisha kiuchumi kupitia biashara, huduma kwa wafanyakazi wa mradi.

“Tumejionea wenyewe, tunawatoa hofu hofu wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huu kwa sababu Serikali inatimiza wajibu kwa kuhakikisha unatekelezwa kwa ubora na wakati,” aliongeza.

Aliuagiza uongozi wa TRC na mamlaka zote za Serikali zinazohusika kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati, ubora unaolingana na thamani halisi ya fedha.

“Mradi huu utarahisisha usafirishaji abiria na mizigo kutoka Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa kwenda Dar es Salaam kwa muda mfupi.

“Wataalama wametueleza kuwa, wanaotoka Mwanza asubuhi wataweza kula chakula cha mchana jijini Dar es Salaam, haya ni mapinduzi makubwa katika sekta ya usafirishaji nchini,” alisema Silaa.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here