Home KITAIFA ZABUNI UUZAJI MRADI WA DEGE BADO IPO KATIKA MCHAKATO HAUJAKAMILIKA-MSOMBA

ZABUNI UUZAJI MRADI WA DEGE BADO IPO KATIKA MCHAKATO HAUJAKAMILIKA-MSOMBA

Google search engine
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba

Na MWANDISHI WETU

-BEST MEDIA, DODOMA

ZABUNI iliyotangazwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya kuuza mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni, Dar es Salaam, bado ipo katika mchakato.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Mfuko kwa mwaka wa fedha 2022/23 katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.

Amesema mradi huo uliamuliwa uuzwe baada ya kufanyika tathimini mwaka 2020 na kwamba kuuzwa kwa mradi huo kutarudisha gharama  zilizotumika.

“Hivi sasa tulitangaza Zabuni ambayo bado ipo katika mchakato na endapo ikatokea kwamba hatujapata mtu ambaye amefika bei ya kurudisha ile gharama maana yake ni kuwa tutatangaza tena kwa mara nyingine,” amefafanua.

Amesema kwa jinsi ambavyo wawekezaji wanavyoongezeka nchini wataweza kununua mradi huo katika kiwango ambacho kitakuwa na manufaa kwa Mfuko.

Mshomba amesema kuuzwa kwa mradi huo kutakuwa na faida kwa wanachama na Taifa kwa ujumla kwa maana kutaepusha hasara ambazo Mfuko ungepata kutokana na kuendelea nao.

Masha aliwahakikishia wanachama kuwa Mfuko upo salama na kwamba thamani ya Mfuko imeongezeka na kufikia Sh trilioni 6.6 mwezi Desemba 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 36 kutoka Sh trilioni 4.7 iliyokuwa mwezi Machi, 2021.

“Ongezeko hili linatokana na kuongeza michango ya wanachama pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji, hivyo ukuaji huu wa Mfuko unathibitisha kuwa NSSF ipo imara na endelevu kwa ajili ya utoaji huduma za hifadhi ya jamii nchini,” amesema Mshomba.

Amesema katika mwaka wa fedha unaoishia mwezi Juni 2023, Mfuko unatarajia kukusanya michango ya Sh trilioni 1.6 ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na michango ya Sh trilioni 1.4 kwa mwaka 2021/22.

Mshomba amesema mapato yatokanayo na uwekezaji kwa mwaka 2022/23 yanatarajiwa kuendelea kuwa Sh bilioni 700 kiasi ambacho ni ongezeko kubwa ukilinganisha na miaka ya hivi karibuni ambapo mapato hayo yalikuwa chini ya Sh bilioni 500.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here