Home KITAIFA BILIONEA LAIZER ANYAN’GANYWA NJIA YA MGODI ULIOVUNJA REKODI MIRERANI KWA KUTOA MADINI...

BILIONEA LAIZER ANYAN’GANYWA NJIA YA MGODI ULIOVUNJA REKODI MIRERANI KWA KUTOA MADINI MAKUBWA

Google search engine

*WACHIMBAJI WAKE 580 SASA WAKOSA AJIRA, RAIS SAMIA AOMBWA KUINGILIA KATI

Na MWADISHI WETU

MIRERANI, MANYARA

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameombwa kuingilia kati, mgogoro wa kufungwa njia ya mgodi wa Bilionea Saniniu Laizer (pichani juu), ambao  mwaka 2020 ulivunja rekodi ya kutoa madini makubwa zaidi ya Tanzanite tangu kugunduliwa madini hayo miaka zaidi ya 50 iliyopita .

Kutokana na kufungwa njia ya mgodi huo, tangu Desemba 10, 2023 uliosajiliwa  ML 543/2015 vijana 580 waliokuwa wanafanyakazi wamekosa ajira huku, pia serikali ikipoteza mapato ikiwepo kodi zaidi ya milioni 500 hadi sasa.

Juni 23 mwaka 2020 Laizer alitangazwa kuvunja rekodi ya upatikanaji madini Mererani, baada ya kupata mawe ya madini makubwa moja likiwa na kilo 9.27 na jingine kilo 5.103 ambayo yalinunuliwa na serikali kwa zaidi ya Shilingi bilioni 7.8.

Mchimbaji huyo, baadae alipata jiwe jingine  lenye uzito wa kilo 6.33 na kuiuzia serikali kiasi cha Shilingi bilioni  4.86 ambapo kaika mauzo hayo makubwa ya madini hayo, Serikali iliweza kupata kodi na malipo mengine zaidi ya Shilingi milioni  800.

Kutokana na hali hiyo, tangu kupatikana madini hayo, mchimbaji huyo, alikuwa akifatiliwa na wa wachimbaji wengine na kutafuta njia ambayo ametumia kufikia madini hayo, lakini hata hivyo wamekuwa wakikwama kwani amechimba zaidi ya kilomita 1.5 kufuata mikondo ya madini  na sasa  waendeshaji wa mgodi wa Kitalu C wamevamia na “kuteka” njia ya mgodi huo na kudai ipo katika eneo lao.

Bilionea Laizer akizungumzia kupokonywa njia ya mgodi wake, amesema bado anaimani kubwa na Serikali itamtendea haki kwani ametumia mabilioni ya fedha kuchimba madini katika njia hiyo na amekuwa akishirikiana na serikali kwa miaka yake yote ya uchimbaji wake.

“Mimi napenda haki, tangu nimeanza kuchimba nimekuwa na serikali na maafisa wa madini wanajua  njia hii ambayo nachimba miaka yote ,hawajawahi kusema nivunja sheria. Kwani tumekuwa nao, kodi nimekuwa naongoza kwa kulipa na kusaidia jamii hadi kujenga shule sasa ambacho kimetokea namshitakia Mungu lakini najua haki yangu ipo siku itapatikana”amesema

Meneja msaidizi wa mgodi huo, Paulo Jacob amesema njia muhimu ya mgodi huo, ambao ulikuwa unazalisha imefungwa na  kampuni ya Franone Minning and Gems  Ltd, ambayo imekodishwa na serikali kuendesha eneo la kitalu C.

Jocob amesema wameshangazwa na kufungwa njia ya mgodi huo, ambao ulikuwa umbali za zaidi ya mita 700 chini ya ardhi,kwani hawajawahi kutobozana na mgodi wa Kitalu C  na hawajawahi kuna na mgogoro kwa miaka zaidi ya mitano.

“Sisi tumeanza kuchimba muda mrefu, lakini ilikuwa jumapili usiku desemba 10 mwaka jana, wachimbaji wa Franone walivamia mgodi wetu, baada ya kupitia katika mgodi ya  Tanzanite Explores Ltd ambao tunapakana nao,”amesema

Amesema baada ya kuvamia mgodi huo, waliziba njia na wamezua vifaa vyao vya kazi na mashine zote, vifaa ambavyo ni mashine za kuingiza hewa mgodini( moter 6, Gear box 6, blower, Diggers, mfumo wa waya za umeme, nyundo, tindo na vingine kadhaa vikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 500.

Amesema licha ya kuandika barua za malalamiko, ofisi za madini hadi wizara ya madini bila majibu na  Februari 29 mwaka huu, walituma barua nyingine kwa Afisa madini mkazi Mererani, Nchagwa Marwa kutaka kupatikana suluhu ya mgogoro huo hawajawahi kuhojiwa wala kupewa majibu yoyote.

“Hawataki kujibu barua na wanatujibu kwa maneno tukae kumalizana na Franone sasa imekuwa ngumu kupata suluhu ya mgogoro huu,” amesema

Hata hiyo, Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Wachimbaji Madini Mirerani, Jeremiah Sumari amesema anaiomba serikali kutenda haki katika mgogoro huo na kujali maisha ya maelfu ya wakazi wa Mirerani ambao sasa wanataabika kutokana na kukosa kazi ya kuchimba madini.

AFISA MADINI ARUKA KIMANGA

Kutokana na sakata hilo, alipotafutwa Afisa Madini Mkazi Mirerani, Nchagwa Marwa alikiri  kupokea  barua ya malalamiko ya Bilionea Saniniu Laizer lakini hata hivyo, amesema suala hilo linashughulikiwa na Katibu wa Tume ya Madini.

“Mimi sio msemaji wa jambo hili, naomba mumtafute Katibu Tume ya Madini ndio anaweza kuzungumzia,” amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Franone Onesmo Mbise, amekuwa akiwatuhumu  wachimbaji  wadogo wanachimba eneo lake la Kitalu C.

WACHIMBAJI, WANAWAKE MERERANI “WALIA” 

Baadhi ya wachimbaji wadogo na Wakazi wa Mererani, wameomba Rais kuingilia kati kutatua mgogoro huo, kwani sasa mji wa Mirerani, uko katika taharukikutokana na vijana zaidi ya 1000 kukosa ajira, kukosekana fedha na hivyo suala la wizi linaripoiwa kushamiri katika eneo hilo.

Wakazi wa Mirerani  Zaituni Said, amesema wanawake na vijana wamekuwa waathirika wakubwa baada ya kufungwa migodi ya wachimbaji wadogo ambayo inazalisha kwa tuhuma kuwa inachimba eneo la Kitalu C.

“Tunamuomba Mama Samia Rais wetu, aingilie kati kumaliza mgogoro huu, kwani tunajua kuna vigogo wapo nyuma ya mgogoro huu kwa maslahi yao, mji wa Mirerani unakufa, wizi, umeongezeka, wanawake wametelekezewa familia kwa sababu hakuna fedha tena,” amesema

Kwa upande wake Kanaeli Minja amesema kwa miaka yote mji wa Mirerani unategemea  wachimbaji wadogo lakini tangu migodi yao kufungwa kwa tuhuma za kuchimba eneo la kitalu C, maisha yamekuwa magumu sana Mererani.

“Tunalia na Rais kwani tunajua kuna watu wapo nyuma ya mgogoro huu, mbona hawa ambao wanabebwa hatuelezwi hata kodi ambayo wanalipa serikalini, hakuna mapato yanayojulikana, huyo Laizer ndiye dunia nzima wanajua amevunja rekodi ya kupata madini makubwa hao wanaobebwa madini yao yapo wapi,” amesema

Amesema wanawake wa Mererani ndio waathirika wakubwa na wanajipanga kufanya maandamano ya amani hadi mgodini ili kulia haki ipatikane kwa wachimbaji wote na wanawake na vijana wanufaike kuliko sasa mji wa Mererani umegeuka magofu, watu wanahama kutokana na hali ngumu ya maisha.

Mchimbaji wa mgodi huo, Erick Sekawa amesema kuwa kufungwa kwa njia ya mgodi huo, kumewathiri kwani wanashindwa kuendesha familia na wanashangazwa na ukimya wa Wizara ya Madini kwani tangu tukio kutokea hadi sasa hawajawahi kwenda katika mgodi huo kupima na kujua ukweli.

“Tunajua ni mchezo mchafu lakini tunaumia sisi vijana tunashindwa kusomesha watoto, maisha yamekuwa magumu sana,” amesema

Wachimbaji Saimon Siriya na Sinyoki Laizer, wameomba Serikali kuingilia kati mgogoro huo ili kuokoa maisha ya maelfu ya watu, kuliko kutetea mgodi mmoja ambao haunufaishi wananchi wengi.

“Tunaomba Serikali ije kukaa na wachimbaji wadogo, kutatua migogoro Mirerani imekuwa shamba la bibi sisi, wakazi wa Mirerani hatunufaiki na madini kwa sasa,” amesema.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here