Home KITAIFA REA YATOA MWONGOZO UWEZESHAJI UJENZI VITUO VIDOGO VYA MAFUTA VIJIJINI

REA YATOA MWONGOZO UWEZESHAJI UJENZI VITUO VIDOGO VYA MAFUTA VIJIJINI

Google search engine
Mhandisi Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Kelvin Tarimo, akiwaeleza Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Ruvuma, dhamira ya Serikali kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (Dizeli na Petroli) maeneo ya vijijini. Alikuwa akiwasilisha mada katika Baraza hilo Oktoba 5 mwaka huu kwa mwaliko wa Naibu Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Ruvuma, Judith Kapinga.

VERONICA SIMBA NA ISSA SABUNI – REA

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imedhamiria kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vipya vidogo vya gharama nafuu vya bidhaa za mafuta (Dizeli na Petroli) maeneo ya vijijini ili kuondosha njia zisizo salama za uhifadhi wa mafuta hayo.

Hayo yamesemwa na Mhandisi Miradi kutoka REA, Kelvin Tarimo wakati akitoa semina kwa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma, Oktoba 5 mwaka huu kwa mwaliko wa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga.

Akizungumza na Wajumbe wa Baraza hilo, Mhandisi Tarimo alieleza mambo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa ujenzi wa vituo hivyo kwa wale watakaokidhi vigezo na kupata mkopo wa kuvijenga.

Alisema kuwa pamoja na mambo mengine, mwongozo huo unaainisha bayana vigezo kwa mwombaji wa mkopo ambavyo vimegawanyika katika makundi mawili; kiufundi na kifedha.

Mhandisi Tarimo alivitaja baadhi ya vigezo vya kiufundi kwa mwombaji kuwa ni pamoja na mtu binafsi au kikundi cha wajasiriamali kijijini kilichosajiliwa na Mamlaka husika au Serikali ya kijiji kuwa na kibali cha ujenzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Kigezo kingine ni mwombaji kuwasilisha kwa REA barua ya maombi ya mkopo wa ujenzi wa kituo au vituo vipya tu na siyo vinavyohitaji ukarabati au vilivyoanza kujengwa.

Aidha, mwombaji atatakiwa kuwa na barua ya uthibitisho kutoka Halmashauri ya kijiji na Wilaya inayomruhusu kuendesha biashara ya kituo cha mafuta katika eneo aliloomba pamoja na kuwa na namba ya mlipa kodi (TIN Namba) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Pia, alieleza kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na uthibitisho wa umiliki wa ardhi (Hati Miliki ya ardhi au Hati za kimila au uthibitisho wa umiliki wa ardhi) kutoka kwa Halmashauri ya Kijiji au Wilaya.

Kingine ni kibali cha ujenzi kutoka Mamlaka husika pamoja na kujaza fomu ya kuonesha namna anavyokusudia kufanya biashara ya mafuta.

Akieleza zaidi, Mhandisi Tarimo alisema fedha hizo za Mradi zitakazotolewa kama mkopo, ni sehemu ya juhudi za Serikali zinazolenga kuzuia kuhifadhi mafuta ndani ya nyumba kwa kutumia mapipa na chupa za plastiki katika kuuza mafuta ya petroli na dizeli kwa watumiaji wadogo kama vile waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda katika maeneo ya vijijini.

“Hii ni kutokana na kukua na kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa hizi katika shughuli za maendeleo maeneo ya vijijini,” alisema.

Kiasi cha mkopo ni Shilingi milioni 75 na riba yake ni asilimia tano ilhali marejesho yake ni hadi kipindi cha miaka saba.

Mhandisi Tarimo ametoa hamasa kwa wananchi wote wenye nia kutembelea tovuti ya Wakala wa Nishati Vijijini ambayo ni www.rea.go.tz ili kusoma Mwongozo kamili wa utoaji na usimamizi wa mkopo wa uwezeshaji wa ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta (petroli na dizeli) vijijini.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here