Home KITAIFA DK. BITEKO APELEKA SHANGWE ZA UMEME KIJIJI CHA IHAKO, BUKOMBE

DK. BITEKO APELEKA SHANGWE ZA UMEME KIJIJI CHA IHAKO, BUKOMBE

Google search engine

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Ihako wilayani Bukombe Mkoa wa Geita mara baada ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho tarehe 26 Septemba, 2023.

Moja ya nyumba iliyounganishwa na umeme katika Kijiji cha Ihako
wilayani Bukombe mkoani Geita.

TERESIA MHAGAMA NA GODFREY LULINGA

-GEITA

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameanza kazi ya kuwasha umeme vijijini ambapo  leo  amewasha umeme katika Kijiji cha Ihako, wilayani Bukombe mkoani Geita na hivyo kuwezesha wananchi katika kijiji hicho kuanza  kutumia rasmi nishati hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho, Dkt. Biteko amepongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri ya  kupeleka umeme vijijini ikiwemo kijiji cha Ihako na kuelekeza kuwa, sasa mwendo ni wa mchakamchaka kupeleka umeme kwa wananchi wote waliopo vijijini.

“REA nendeni vijijini, muda wa kufanya vikao kwenye maukumbi makubwa, au makao makuu ya miji hatutaki, tunataka tuwaone mnaenda vijijini kupeleka umeme, nyie ni Wakala wa Nishati Vijijini siyo Wakala wa umeme mijini, vikao vyenu viwe na wananchi na magari yenu yapite humo wanamopita wananchi wenye maisha ya kawaida kabisa, ” amesisitiza Dk. Biteko

Ameongeza kuwa, Serikali inataka kuona shuguli za kupeleka na kuwasha umeme vijijini zinatokea, na kwamba umeme huo uingie kwenye nyumba zote bila kubagua kwani kila mwananchi anahitaji umeme.

Aidha ameelekeza kuwa, mahali penye changamoto za umeme zitatuliwe kwa haraka na si kumsubiri, Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kutatua changamoto wakati wa ziara zake  wakati wasaidizi wake wapo.

Amesema kuwa fedha za kupeleka umeme vijijini zipo ambazo zimechangiwa na wananchi, Serikali na wadau wa maendeleo hivyo hakuna sababu ya kukwamisha miradi ya umeme nchini.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, amesema kuwa,  Serikali inataka ione wananchi wanatumia nishati hiyo  na kwamba REA waweke mpango ili mitungi ya gesi iwafikie wananchi wa kawaida nchini na hivyo kuwaondolea matumizi ya nishati ambayo si salama.

Vilevile amesema kuwa, Serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kupata umeme wa kutosha kutoka vyanzo vya umeme ikiwemo Mradi wa Julius Nyerere (MW 2115) ambao utaongeza kiasi kikubwa cha umeme kwenye gridi ya Taifa na hivyo wadau wa umeme watapata umeme wa kutosha  ikiwemo viwanda, wachimbaji wadogo na wenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema kuwa, Mkoa wa Geita una jumla ya Vijiji 461 ambapo vijiji 399 sawa na asilimia 86.6 vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA Awamu ya Tatu mzunguko kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.

Amesema kuwa, REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali mkoani Geita ambapo wakandarasi wapo maeneo ya miradi wanaendelea na kazi na kuitaja miradi inayoendelea kuwa ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, mradi wa kupeleka umeme pembezoni mwa miji Awamu ya Tatu, mradi wa kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo pamoja na mradi wa kupeleka umeme kwenye vituo vya afya na pampu za maji.

Google search engine
Previous articleKAPINGA: KAZI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI MWISHO DESEMBA 2023
Next articleDK. BITEKO AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI KAGERA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here