Home KITAIFA NSSF YAZIDI KUNGA’RA, MCHANGO WA WANACHAMA WAFIKISHA TRILIONI 1.7/-, THAMANI YA MFUKO...

NSSF YAZIDI KUNGA’RA, MCHANGO WA WANACHAMA WAFIKISHA TRILIONI 1.7/-, THAMANI YA MFUKO YAKUA

Google search engine

*WAMSHUKURU RAIS Dk. SAMIA KUWA CHACHU YA MAGEUZI NA MAFANIO YAO

*MRADI WA DEGE-ECO VILLAGE SASA KUUZWA, MNUNUZI KUJULIKANA OKTOBA MWAKA HUU

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, akifafanua mambo mbele ya wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) leo Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, akijadiliana jambo la Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Erick Mkuti
Mkuu wa Kitengo cha Mwasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Erick Mkuti (kushoto), akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile kwenye uliowakutanisha Wahariri na uongozi wa NSSF leo Septemba 25, 2023 Jijini Dar es Salaam

Meneja Uhusiano wa NSSF,Lulu Mengele, akizungumza jambo kwwenye mkutano uratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kuwakutanisha Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, akifafanua mambo mbele ya wahariri wa vyombo vya habari (hawapo pichani) leo Septemba 25, 2023 jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza jambo katika mkutano huo leo, Septemba 25, 2023
Baadhi ya Wakurugenzi wa idara mbalimbali wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wakisikiliza majadiliano kwenye mkutano huo
Baadhi ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa kwenye mkutano huo leo Septemba 25, 2023

Na MWANDISHI WETU

-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeweka wazi mafanikio yake ikiwamo hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuweka mazingira rafiki ya uwezaji jambo ambalo limewasaidia kusajili namba kubwa ya wanachama wake ambao wamesaidia kukuza mchango wa mfuko huo na kufikia Sh Trilioni 1.7 katika hesabu zake ambazo zinakaguzliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hayo yamesemwa leo Oktoba 25, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, katika semina iliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari, ambapo amesema kuwa hatua hiyo imewasaidia kuongezeka kwa makusanyo hadi kufikia Juni 30, 2023 wamefanikiwa kufikia kiasi cha Sh Trilioni 1.7 kutoka Sh bilioni 97.67 iliyofikiwa tarehe 1 Machi 2021 hadi kufikia bilioni 143.05 kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30 2023.

Amesema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa waajiri wanaowasilisha michango kwa wakati na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara kwa sekta binafsi.

“Aidha, makusanyo ya michango kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 43 hadi kufikia Shilingi bilioni 1,718.28 katika mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2023 ukilinganisha na bilioni 1,201.05 zilizokusanywa,” amesema Mshomba

MRADI WA DEGE-ECO VILLAGE

Akizungumzia mradi huo, Mkurugenzi huyo wa NSSF, amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, mfuko huo unatarajia kuuza mradi wa Dege Eco Village wenye eneo la ekari 302, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambapo mradi huo una nyumba 3,750 zilizokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi.

“Mradi huu umeuzwa kama ulivyo, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Bodi ya Mfuko na Serikali ili kurudisha fedha za wanachama zilizowekezwa awali katika mradi huu.

“Kwa sasa Mfuko kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali unakamlisha taratibu za zabuni baada ya kukamilika kwa hatua ya tathmini ya zabuni na maafikiano ya bei. Matarajio ni kusainiwa kwa mkataba wa mauzo ya mradi huu kabla ya tarehe 31 Oktoba 2023,” amesema

MRADI WA KIWANDA CHA SUKARI, MKULAZI

Akizungumzia mradi mradi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi, amesema kuwa mradi huo uliopo Mbigiri Wilaya ya Kilosa, unamilikiwa kwa ubia katiya NSSF asilimia 96 na Jeshi la Magereza asilimia 4.

“Ukubwa wa shamba lamradi huu ni hekta 4,856 (ekari 12,000) na kiwanda kinatarajiwakuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka. Jumla ya gharama zamradi ikijumuishwa na thamani ya ardhi inatarajiwa kuwa shilingibilioni 344.47.

“Hadi kufikia 30 Juni 2023, utekelezaji wa mradi (work progress) kwa upande wa mashamba ya miwa ulifikia asilimia 86 na upande wa kiwanda (factory) ulifikia asilimia 93. Gharama zilizokwishatumika katika mradi huu ni asilimia 88 ya gharama zote na mradi huu unatarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji wa sukari mwishoni mwa Oktoba 2023.

“Mradi huu utaongeza mapato ya mfuko, uzalishaji wa sukari nchini, mapato ya kodi wa Serikali na kuongeza ajira zipatazo 11,315,” amesema

MAFANIKIO HADI KUFIKIA JUNI 30, 2023

Mshomba, amesema kuwa katika kipindi husika, mali zote za Mfuko zimeongezeka kwa Shilingi bilioni 2,847.43 kutoka Shilingi bilioni 5,218.00 iliyofikiwa katika kipindi kilichoishia Machi 1, 2021 hadi kufikia shilingi bilioni 8,065.43 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023.

“Ongezeko hili la takribani asilimia 55 limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa mapato yanayotokana na michango, uwekezaji, udhibiti wa mapato pamoja na mifumo ya udhibiti wa fedha.

“Aidha, kati ya mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2021 na mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2023, thamani ya mali zote za Mfuko imekua kwa asilimia 51 na kufikia Shilingi 8,065.43 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023 ukilinganisha na Shilingi 5,325.25 iliyofikiwa katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 2021.

“Thamani ya Mfuko iliongezeka kwa Shilingi bilioni 2,773.93 kutoka Shilingi bilioni 4,837.93 iliyofikiwa katika kipindi kilichoishia Machi1, 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 7,611.86 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023. Ongezeko hili la takribani asilimia 57, limechangiwa na kuongezeka kwa mapato yanayotokana na michango, kukua kwa vitega uchumi vya Mfuko pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji.

HALI YA UTENDAJI WA MFUKO

Mshomba, amesema kuwa mfuko huo ulikuwa una jumla ya wanachama 874,082 ambapo michango kwa mwezi ilikuwa Sh bilioni 97.67 huku mapato ya uwekezaji kwa mwezi yalikuwa Sh bilioni 37.35 ambapo kila wakati yamekuwa yakiongezeka kutokana na tija inayopatikana hasa kwa wanachama wake.

Mkurugenzi huyo wa NSSF, amesema kuwa malipo ya mafao kwa mwezi yalikuwa Sh bilioni 50.58 huku thamani ya vitega uchumi ilikuwa Sh bilioni 3,395.46, mali za mfuko (total assets) zikiwa Sh bilioni 5,218.00 na thamani ya Mfuko (Fund size) ilikuwa Sh bilioni 4,837.93,” amesema

UTENDAJI WA MFUKO

Mkurugenzi Mshomba, amesema kuwa kati ya Machi 1, 2021 na 30 Juni 2023, mfuko uliandikisha jumla ya wanachama 547,882 na idadi ya wanachama wachangiaji iliongezeka kwa asilimia 36 kutoka 874,082 hadi kufikia wanachama 1,189,222 Juni 30, mwaka ambapo hali hiyo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikichangiwa na mkakati wa Serikali wa kuvutia wawekezaji, pamoja na utekelezaji wa mpango wa Mfuko katika uandikishaji wanachama.

Aidha amesema kuwa wanachama wachangiaji katika mfuko huo wameongezeka kwa asilimia 26 hadi kufikia wanachama wachangiaji 1,189,222 Juni 30 2023 ikilinganishwa na wanachama wachangiaji 945,029 waliofikiwa Juni 30, 2021.

UWEKEZAJI NA THAMANI YAKE

Mkurugenzi huyo wa NSS amesema kuwa uwekezaji wa Mfuko (investment portfolio) iliongezeka kwa asilimia 111 kutoka Sh bilioni 3,395.46 Machi1,2021 hadi kufikia Sh bilioni 7,153.23 Juni 30, 2023 hali ambayo imekuwa ikichangiwa na kukua kwa thamani ya vitegauchumi, michango ya wanachama na mapato ya uwekezaji.

“Thamani ya vitegauchumi vya Mfuko imekua kwa asilimia 55 hadi kufikia Shilingi bilioni 7,153.23 Juni 30, 2023 kutoka Shilingi bilioni 4,622.25 zilizofikiwa Juni 30, 2021,” amesema Mshomba

MAPATO YATOKANAYO NA UWEKEZAJI

Mshomba, amesema kuwa wastani wa mapato ya uwekezaji kwa mwezi katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023, yalifika Sh bilioni 72.06 ikiwa ni ongezeko la asilimia 92 ukilinganisha na Sh bilioni 37.35 zilizokusanywa Machi 2021.

“Mapato halisi (real rate of return on investment) ya Mfuko yameongezeka kutoka wastani wa asilimia 3.31 mwezi Machi 2021, hadi kufikia asilimia 5.32 kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2023.

“Mapato ya uwekezaji kwa mwaka yameongezeka kwa asilimia 93 na kufikia Shilingi bilioni 864.76 katika mwaka wa fedha ulioishia 30 Juni 2023 ukilinganisha na Shiliongi bilioni 448.17 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 30 Juni 2021,” amesema

ULIPAJI WA MAFAO

Kutokana na mafanikio hayo Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF, amesema kuwa katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023 Mfuko ulilipa Sh bilioni 61.93 kwa mwezi kama mafao kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ukilinganisha na Sh bilioni 50.58 zilizolipwa kwa mwezi kipindi kilichoishia Machi Mosi, 2021.

“Ongezeko hili lilichangiwa na kuongezeka kwa madai ya fao la upotevu wa ajira (unemployment benefit) na mkupuo maalum (special lumpsum). Aidha, malipo ya mwaka ya mafao kwa wanufaika mbalimbali wa Mfuko yaliongezeka kwa asilimia 25 nakufikia Shilingi bilioni 743.17 katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023 ukilinganisha na Shilingi bilioni 594.33 zilizolipwa katika mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, 2021,” amesema

CHANGAMOTO ZILIZOKUWEPO

Akizungumzia changamoto ndani ya NSSF, Mshomba, amesema kuwa kutowasilishwa kwa michango ya wanachama kwa wakati, inayopelekea ufinyu wa makusanyo na uwekezaji na mapato yatokanayo na uwekezaji

“Kusimama kwa miradi ya uwekezaji kwa muda mrefu kulikosababisha kutokuchangia katika mapato ya Mfuko uchache wa mifumo na matumizi ya Tehama uliosababisha kupungua kwa ufanisi na udhibiti wa mapato.

UANZISHWAJI NA SHERIA YA MFUKO

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulianzishwa mwaka 1964 kama kitengo ndani yaWizara ya Kazi kinachoshughulikia mafao ya wafanyakazi baada ya kustaafu. Mwaka 1975, kitengo hicho kiliboreshwa na kuwa taasisi inayojitegemea iliyoitwa “National Provident Fund” (NPF).

Aidha amesema kuwa maboresho zaidi yalifanyika mwaka 1997, ambapo Sheria Na. 28 ilitungwa na kuibadili NPF kuwa Mfuko wa Pensheni, hivyo kuwezesha kuwa na wigo mpana wa kutoa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi.

Mnamo mwaka 2018 Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii yaliyosababisha kurekebishwa kwa Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (The National Social Security Fund) Sura ya 50 na kuifanya NSSF kuwa Mfuko pekee unaohudumia hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na wale wa sekta isiyo rasmi nchini.

MABORESHO KATIKA MIFUMO YA UTENDAJI

Mfuko umefanya maboresho mbalimbali ya mifumo ya utendaji kupitia Tehama, ambapo baadhi ya maboresho yaliyofanyika ni kuanzishwa kwa mfumo wa kujihudumia kwa ajili ya Waajiri (Employer Portal), Mfumo wa kujihudumia kwa ajili ya Wanachama (Member Portal) pamoja na mfumo wa ukaguzi wa wanachama (Inspector Portal).

“Mfuko umeendelea kuimarisha mifumo na usimamizi wa fedha ili kuepuka mianya ya upotevu wa fedha, kuendelea kumudu gharama za uendeshaji pamoja na kulipa mafao stahiki kwa wastaafu na wanufaika wengine,” amesema Mshomba

HATI SAFI

“Kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi, Mfuko umekuwa ukipata Hati Safi (unqualified reports) kutokana na kaguzi zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Hati Safi za mkaguzi zinathibitisha kuwa fedha za wanachama zipo salama.

MPANGO WA TAIFA WA SEKTA ISIYO RASMI (NISS)

Amesema Mfuko umefanya mapitio ya Mpango wa utoaji wa huduma za Hifadhi ya Jamii katika sekta isiyo rasmi (NISS). Hii ilitokana na Mpango wa NISS kukosa mafao na huduma za zinazowavutia wananchi walio katika sekta isiyo rasmi kujiunga na mfuko.

Mshomba, amesema maboresho ya Mpango huo yanalenga kukidhi haja na matakwa ya wananchi ambapo kuandaliwa na kuidhinishwa kwa muongozo wa uendeshaji wa Mpango wa utoaji wa huduma za Hifadhi ya Jamii katika sekta isiyo rasmi (NISS) utasaidia kuongeza wigo wa wanachama, mapato kwa Mfuko na kutoa fursa mbalimbali kwa sekta isiyo rasmi.

Amsema mpango wa NISS ulioboreshwa unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na kuanza kutumika kabla ya Julai 2024.

UTEKELEZAJI WA MIRADI ILIYOKUWA IMESIMAMA

Amesema mfuko unatekeleza miradi mitano (5) ambayo ni miradi ya nyumba za makazi za Dungu, Toangoma, Mtoni Kijichi, jengo la kibiashara na makazi la Mzizima Towers na Hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano, Mwanza.

Amesema kuwa changamoto na kasoro za kizabuni na kimikataba zilizokuwepo zilipelekea miradi hii kusimama mwaka 2016.

“Miradi hii imepitia hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa mapitio (review) na kufanyiwa kaguzi maalum ikiwepo ile ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) iliyokamilika mwishoni mwa mwaka 2020.

“Katika kipindi kilichoanzia tarehe 1 Machi, 2021, Mfuko ulitatua changamoto zilizokuwepo na kwa sasa utekelezaji wa miradi yoteunaendelea na miradi hii inatarajia kukamilika kati ya Juni na Septemba 2024.

SABABU ZA UKUAJI WA KASI WA MFUKO

Mshomba, amesema kuwa ukuaji huu mzuri wa mfuko wa NSSF umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la michango na mapato yatokanayo na uwekezaji.

Amesema katika kipindi husika, makusanyo ya michango yameongezeka kwa takribani asilimia 45 na mapato yatokanayo na uwekezaji wa Mfuko yamekua kwa zaidi ya asilimia 90.

Google search engine
Previous articleNMB JAMII BOND: HATIFUNGANI MPYA KWA UWEKEZAJI WENYE TIJA
Next articleHABARI PICHA: RAIS SAMIA ALIVYOPOKEA HATI ZA MABALOZI WA NCHI MBALIMBALI LEO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here